Katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas amefunga rasmi mafunzo ya
nadharia na vitendo ya Uongozi kwa Maafisa na Askari 311 wa Jeshi la Uhifadhi
kutoka TANAPA na Mafunzo ya Awali ya Askari 369 wa TFS leo, Oktoba 25, 2025 katika Chuo cha Mafunzo cha
Jeshi la Uhifadhi Mlele mkoani Katavi.
Akizungumza
wakati wa kufunga mafunzo hayo, Dkt.Hassan Abbas aliwataka wahitimu hao
kutekeleza mafunzo waliyoyapata kwa vitendo, kushirikiana kazini, na kuongeza
uwajibikaji ili kuleta tija kwa Taifa.
Awali,
Dkt. Abbas alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa ajira
kwa vijana wa Tanzania katika sekta ya Maliasili na sekta zingine nchini.
"Tumshukuru
Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri Askari 311 na
wengine zaidi ya 500 wanaokuja kupata mafunzo hapa pamoja na kuruhusu
kupandishwa vyeo kwa Maafisa na Askari na niwatake vijana nchini kuchangamkia
fursa ya ajira zinazotolewa katika sekta ya Maliasili na sekta zingine ambazo
zinaendelea kutolewa na serikali".
Naye,
Kamishna wa Uhifadhi, TFS - Prof. Dos Santos Silayo aliwapongeza wahitimu hao
kwa kumaliza mafunzo yao na kuwataka kutumia mafunzo waliyoyapata katika kuendeleza
sekta ya Uhifadhi na Utalii nchini.
Naibu
Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa
alibainisha kuwa mafunzo waliyopatiwa Maafisa na Askari yanawajengea uwezo
katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika kuhifadhi Rasilimali za
Wanyamapori na Misitu nchini.
"Mafunzo
yanayotolewa hapa Mlele yanawajengea uwezo Maafisa na Askari wa Jeshi la
Uhifadhi katika kutekeleza jukumu la ulinzi wa rasilimali za Taifa kwa niaba ya
watanzania. Sisi kama viongozi wao tunaahidi kuwasimamia vyema na kwenda
kutimiza kiapo chao kwa asilimia mia moja."
"Mafunzo
haya ni muendelezo wa Jeshi letu kuimarika kwa ushirikiano na Jeshi la Wananchi
(JWTZ), Jeshi la Polisi,na vyombo vingine vya Usalama ni ahadi yetu kuwa
tutafanya kazi usiku na mchana ili kulinda Maliasili na kuboresha huduma kwa
watalii wanaotembelea maeneo yetu ya vivutio" alisema
Kamisha Mwishawa.
Na.
Edmund Salaho -Mlele - Katavi



0 Maoni