Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum
Wakili Amon Mpanju amewaasa Maafisa Maendeleo ya Jamii mkoani Geita waliopatiwa
pikipiki ambazo zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita kuzitunza pikipiki hizo na kuzitumia kwa
malengo yaliyokusudiwa na sio shughuli zao binafsi.
Wakili
Mpanju ametoa wito huo tarehe 24 Oktoba 2024 alipokuwa akikabidhi pikipiki nane
(8) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata za Muganza, Kigongo, Lwamgasa,
Shabaka, Uyovu, Namonge, Masumbwe na Lulembela katika hafla fupi iliyofanyika
katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Wakili
Mpanju ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita
katika kutekeleza matakwa ya kikatiba ya kugatua rasilimali fedha, ushushaji wa
huduma pamoja na watumishi ili kuwafikia wananchi wote walioko katika
vitongoji, vijiji, mitaa na Kata na katika hili ndani ya miaka miwili Sekta ya
Maendeleo ya Jamii imeajiri watumishi zaidi ya elfu moja.
“Serikali
imeona kuajiri wataalam wa Maendeleo ya Jamii kwenye Kata pekee bila kuwapatia
vitendea kazi inakuwa haitoshi kama tunavyojua jiografia ya Nchi yetu ni pana,
kuna baadhi ya wananchi wanaishi mbali na Makao makuu ya Halmashauri. Hivyo
Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao ni wachechemzi na wahamasishaji wakubwa wa
maendeleo ambao wanatakiwa wahakikishe wananchi wanatambua fursa mbalimbali
zinatozolewa na Serikali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu kwa kuwahamasisha
katika maeneo yao." amesema Wakili Mpanju.
Wakili
Mpanju ameongeza kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata wana uwezo, mbinu na
kuamsha ari ya maendeleo katika ngazi ya msingi kwa kutekeleza majukumu
mbalimbali kwa manufaa ya jamii lakini wanahitaji nyenzo za kuwawezesha
kuwafikia wananchi hao. Hivyo katika kutambua hilo Serikali imeweka utaratibu
wa kununua pikipiki kila mwaka, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 imenunua
pikipiki 98 ili kuboresha utendaji kazi wa Maafisa hao wakishirikiana na
wataalam wengine kwenye Kata na kutimiza majukumu yao kiufanisi.
Kwa
upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita Martha Kaloso ameeleza kuwa
Idara ya Maendeleo ya Jamii mkoani humo inakabiliwa na uhaba wa vyombo 131 vya
usafiri kwa wataalam wake katika ngazi ya Kata hali inayopelekea uwajibikaji
hafifu wa kuwafikia wananchi walioko maeneo ya vijiji vya mbali, ufuatiliaji
hafifu wa shughuli za miradi ya maendeleo ya Jamii na ufuatiliaji hafifu wa
mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Nao
Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopokea pikipiki hizo akiweko Afisa Maendeleo ya
Jamii wa Kata ya Namonge Wilaya ya Bukombe Wajama Bwire ametoa shukrani za
dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwakumbuka na kuwapatia pikipiki zitakazowawezesha kutoa
huduma kwa wananchi katika maeneo ambayo yako mbali na makao makuu ya
Halmashauri zao.
Na. Mwandishi Wetu WMJJWM- Geita



0 Maoni