Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imewashirikisha
baadhi ya watalii katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja ambapo wageni hao
wameipongeza mamlaka hiyo kwa kuendelea kuboresha huduma na miundo mbinu ya
utalii.
Wakizungumza katika hafla iliyofanyika kwenye lango
kuu la kuingia Hifadhi ya Ngorongoro eneo la Loduare baadhi ya watalii hao
wamesema kuwa wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo na kusema
wataendelea kuwashawishi wageni wengine kutoka nchi zao kutembelea
Ngorongoro.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi
anayeshughulikia Huduma za Utalii Mariam Kobelo amewahakikishia wageni hao kuwa
mamlaka itaendelea kuboresha huduma zake na kwamba watafanyia kazi kwa ukaribu
maoni yote yatakayotolewa na wateja ili kuendelea kuunga mkono juhudi za
serikali za kuongeza wageni katika sekta ya utalii.
“Tunaitumia wiki hii ya huduma kwa wateja kuendelea
kupokea maoni mbalimbali ya wateja wetu,tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa
tunashughulikia maoni yote yatakayotolewa ili kuunga mkono kwa vitendo juhudi
za serikali yetu za kuboresha utalii nchini,” alisema Mariam.
Wiki ya Huduma kwa wateja ni mahsusi kwa ajili ya
kutoa nafasi kwa watumishi wa sekta mbalimbali kuwasikiliza wateja wao na
kufanyia kazi maoni ya wateja wao.





0 Maoni