Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini vimeendelea
kufanya mazoezi ya pamoja, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni utaratibu wa kawaida
wa kijeshi unaolenga kuimarisha utayari na weledi na wala si mbinu ya kuwatisha
wananchi.
Kauli hii inatolewa kufuatia kuwepo kwa upotoshaji
wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii, unaodai kuwa mazoezi hayo yanatumika
kama vitisho au mbinu za kukandamiza.
Vyombo hivyo vimekiri kuwa kuna propaganda hizo
zisizo na msingi zinazoenezwa mtandaoni zinafanywa kwa lengo la kuchochea hofu
na kuhalalisha maandamano haramu.
Wito umetolewa kwa wananchi wote kupuuza uzushi wa
mitandaoni na kutambua kuwa mazoezi haya ni ngao ya taifa, si tishio kwa
wananchi.
"Huu ndio uthibitisho kwamba Tanzania
inaendelea kuwa nchi ya amani, salama, na thabiti. Mazoezi haya ni kinga yetu
kama taifa," ilihitimisha taarifa hiyo.
Vikosi vya ulinzi vimekumbusha umma kuwa mazoezi
ndiyo shughuli yao ya msingi, na hakuna sababu yoyote kwa wananchi kuwa na
hofu. Lengo la msingi la mazoezi ya pamoja ni kupima uwezo wa vikosi vyote
wakati wa kushughulikia mambo mbalimbali yanayohusu taifa, ikiwamo:Ulinzi wa
mipaka na amani ya taifa;Kukabiliana na maafa (mfano: tetemeko la ardhi,
mafuriko au majanga mengine) na Kudumisha mshikamano wa kiutendaji kati ya
vyombo vyote vya ulinzi.
"Mazoezi haya, yanayojumuisha matembezi ya
pamoja, mafunzo ya viungo, na mazoezi ya kivita, yanaboresha afya za askari,
yanaongeza weledi wa kazi, na kujenga mshikamano wa kikazi," ilisema
taarifa iliyotolewa na vyombo hivyo.
Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimesisitiza kuwa
mazoezi mengi hufanyika hadharani katika barabara na maeneo ya wazi ili
kuonyesha uwazi na kuhakikisha wananchi wanatambua utayari wa vyombo vyao vya
ulinzi.
"Ukweli unabaki palepale: wananchi wengi
wameona kwa macho yao kuwa mazoezi haya ni kielelezo cha utayari wa vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama," ilisisitiza taarifa hiyo.

0 Maoni