INEC yafanya marekebisho ya wapiga kura, vituo vya kupigia kura

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefanya marekebisho ya takwimu za wapiga kura na idadi ya vituo vya kupigia kura vitakavyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kufuatia taarifa rasmi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Marekebisho hayo yametokana na uchakataji wa taarifa za wapiga kura waliopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Zanzibar, ambao umekamilika hivi karibuni.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Oktoba 7, 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima, amesema kuwa jumla ya wapiga kura walioandikishwa kwa sasa ni 37,647,235, wakiwemo 36,650,932 kutoka Tanzania Bara na 996,303 kutoka Zanzibar.

Takwimu za awali zilizotangazwa zilionyesha wapiga kura 37,655,559, hivyo idadi hiyo imepungua kwa watu 8,324 baada ya kufanya marekebisho.

“Katika idadi hiyo, asilimia 50.34 ni wanawake, huku asilimia 49.66 wakiwa ni wanaume,” amesema Kailima.

Kuhusu vituo vya kupigia kura, INEC imesema kuwa kutakuwa na jumla ya vituo 99,895 vitakavyotumika katika uchaguzi huo, ambapo 97,348 vitakuwa Tanzania Bara na 2,547 vitakuwa Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mabadiliko yaliyowasilishwa na ZEC Julai 26, 2025, yameonyesha kuwa Zanzibar ina jumla ya wapiga kura 717,557 watakaopiga kura katika vituo 1,752.

INEC imesema kuwa takwimu hizo mpya zitakabidhiwa rasmi kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo, ili kuwezesha maandalizi ya uangalizi, usimamizi na utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Chapisha Maoni

0 Maoni