WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya
Madini kufanya ufuatiliaji wa makampuni ya madini ambayo yameshilikilia maeneo
kwa muda mrefu lakini hawajayaendeleza mpaka sasa yakiwemo makampuni matatu
wilayani Ruangwa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa makampuni ya Nachu,
Uranex na Paco Gems Ltd yanapaswa kusema hatma ya maeneo waliyoyahodhi kwa muda
mrefu vinginevyo ardhi hiyo itarudishwa kwa wananchi.
Ametoa agizo hilo leo Jumanne (Oktoba 07, 2025)
alipotembelea kampuni ya uchimbaji wa madini Huaer International Limited katika
kijiji cha Ng’au Ruangwa mkoani Lindi.
“Kampuni ya Paco Gems tangu 2009 mpaka leo hakuna
maendeleo, tunatoka Utanex pale Chunyu, wameshalipa fidia tangu 2012 lakini
mpaka leo hii hakuna maendeleo yoyote, ipo kampuni ya Nachu ambayo ilipata
heshima ya kusaini mkataba mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mpaka leo hii wamepotea na hakuna taarifa.”
Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza kampuni ya Huaer
International Limited ambayo imefanikiwa kuanza mchakato wa uwekezaji ndani ya
kipindi kifupi baada ya kupata vibali vyote muhimu.
“Kampuni yako ambayo imeanza ukaguzi mwaka 2024,
ukapata matokeo mwaka huohuo na kuomba vibali mwaka huohuo, leo mmeanza
utekelezaji wa ujenzi na mmefikia hatua hii, ninyi mnapaswa kupongezwa na
mnapaswa kuwa mfano wa makampuni haya mengine tata.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi
wa kampuni hiyo ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya kuzalisha ajira kwa Watanzania kupitia uwekezaji. “Kampuni hii ndiyo
inaanza na inaendelea na ujenzi mtakapokamilisha mtatoa nafasi ya Watanzania na
Wana-Ruangwa kupata ajira hapa.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa vijana wa
Kitanzania waliopata nafasi ya kufanya kazi katika kampuni hiyo kufanya kazi
kwa bidii, weledi, nidhamu na uaminifu “Tunahitaji kuwahakikishia hawa
wawekezaji kwamba tunaajirika na tunaweza kufanya kazi hizi.
Kwa Upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye
ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ameishukuru Serikali kwa
kuendelea kufungua fursa za uwekezaji
kwa mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa
kichocheo cha maendeleo kwa wakazi wa maeneo hayo.
Amesema kuwa uwekezaji wa kampuni ya Huaer utakuwa
ni moja ya fursa kubwa sio tu kwa uchumi wa Wilaya ya Ruangwa au Mkoa wa Lindi
bali Tanzania kwa ujumla.
“Sisi upande wa Mkoa tunaendelea kuahidi kutekeleza
sera zote za uwekezaji ambazo Serikali inaziweka na kuendelea kushirikiana na
wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki ili waendelee kuwa kwa wingi katika mkoa
wetu.”
Thamani ya mradi huo ni dola za
marekani milioni 20.



0 Maoni