Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI
anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila ametembelea na kukagua
maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Utete-Kingupira yenye urefu wa Kilomita 32
inayojengwa kwa kutumia Teknolojia Mbadala ya “Eco-roads” wilayani Rufiji
mkoani Pwani.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mhandisi
Mativila amesema kuwa, katika barabara hiyo Kilomita 2 itawekwa lami na sehemu
inayobakia itawekwa changarawe huku akimtaka Mkandarasi RAPCO Construction Company
kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kabla mvua hazijaanza.
“Nina imani na Mkandarasi huyu kwani amefanya vizuri
katika mradi mwingine wa barabara ya Chumbi-Kiegele, utekelezaji wa kazi hii
umefika asilimia 40, nina amini kazi hii nayo ataikamilisha kwa wakati,
maelekezo ni kwamba Mkandaradi aikimbize kazi hii kabla mvua hazijaanza ili
ikamilike kwa wakati,” amesema.
Aidha, amemtaka Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani
kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati kwani barabara hiyo ni muhimu kwa
usafirishaji wa mazao mbalimbali.
Akisoma taarifa ya mradi, Meneja wa TARURA wilaya ya
Rufiji, Mhandisi Nicholaus Ludigery amesema kuwa mradi huo wenye thamani ya
Shilingi Bilioni 2.5 ni muhimu kwa wana Utete na wana Rufiji kwa ujumla kwani
barabara hiyo inaelekea kwenye hifadhi ya Taifa ya Selous na wananchi wanafanya
shughuli za kilimo cha ufuta, korosho, machungwa na mazao mengine mbalimbali.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo
itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, itarahisisha kuzifikia huduma
za kijamii na pia wakulima wataweza kusafirisha mazao yao
sokoni kwa urahisi.



0 Maoni