WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali
imefanikiwa kutoa kiasi cha shilingi trilioni 3.5 kufikia mwaka 2024 kwa ajili
ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi kutoka shilingi bilioni 904 mwaka 2021.
Amesema kuwa fedha hizo zimewasaidia vijana kupata
mitaji ambayo ambayo imewawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za
uzalishaji mali na hatimaye kuinua vipato vyao pamoja na uchumi wa Taifa.
Amesema hayo leo Ijumaa (Oktoba 10, 2025) Wakati wa
maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa iliyofanyika mkoani Mbeya. Kaulimbiu ya
Maadhimisho hayo ni Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imefanya hivyo
kwa kutambua kuwa Vijana ni nguvu kazi
na ndiyo msingi wa safari ya maendeleo ya Taifa letu. “Vijana wakipewa
nafasi na kuandaliwa ipasavyo, wanaweza kuwa nguzo kuu katika utekelezaji wa
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu
ya Umoja wa Mataifa (SDGs)”.
Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa vijana wamekuwa
nguzo muhimu ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini na wamechangia kwa
kiwango kikubwa katika kilimo, biashara, teknolojia, michezo na sanaa.
“Katika nyanja za ubunifu na teknolojia, vijana
ndiyo vinara wa matumizi ya teknolojia mpya na majukwaa ya kidijitali, ikiwemo
akili mnemba (artificial intelligence) na mifumo ya mawasiliano ya kisasa,
Michango yao imekuwa kichocheo cha mabadiliko chanya katika jamii na uchumi wa
Taifa.”
Pia Mheshimiwa ametoa wito kwa wadau wote
kuhakikisha vijana wanashirikishwa kikamilifu katika ngazi zote za maamuzi na
si tu kama wanufaika wa sera bali pia kama wabunifu na viongozi wa mabadiliko
ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza alipotembelea Banda la VETA , Mheshimiwa
Majaliwa ametoa wito kwa Taasisi hiyo pamoja wadau wengine wa elimu kuwapa kipaumbele
cha mafunzo Wenye Ulemavu pamoja na kuwaandalia nyenzo muhimu za kujifunzia ili
waweze kutumia ujuzi watakaoupata kuongezea kipato.
“Baada ya kutembelea Banda hili nimejifunza kwamba
wapo vijana Wenye Ulemavu wana ujuzi na vipaji, Wazazi tuwe tayari Kuwatoa
watoto wetu Wenye Ulemavu na Taasisi za elimu ziwapokee na kuwapa ujuzi.”
Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Serikali
ya Tanzania inatambua umuhimu wa kundi la Vijana na ndiyo maana inawekeza na
kuthamini mchango na nguvu zao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii
zetu.
“Hii ni rasilimali kubwa ambayo ikielekezwa na
ikijengewa uwezo ipasavyo kupitia vipaji walivyonavyo italeta maendeleo
endelevu, kujenga taifa shindani na lenye ustawi”.




0 Maoni