Kampuni
ya Uuzaji wa Vifaa na Kemikali za Uchenjuaji Madini Chunya, MAPESSA Intertrade
Ltd imeiomba Serikali kuendelea
kuhamasisha wadau na Wawekezaji kuanzisha viwanda vya utengenezaji Vifaa vya
uchenjuaji na kemikali zinazotumika
katika uzalishaji wa madini ya
dhahabu ili viweze kupatikana kwa bei nafuu na kwa urahisi zaidi kwa wachimbaji wadogo.
Akizungumza na Madini Diary hivi karibuni, Mhasibu wa
kampuni hiyo Joyce Ndolela alisema kuwa kutokana na gharama za vifaa hivyo
kubwa kubwa, hupelekea baadhi ya wachimbaji wadogo kushindwa kumudu gharama na
kueleza kwamba, jambo hilo linasababishwa na kutokuwepo kwa viwanda
vinavyozalisha bidhaa hizo nchini na kueleza kuwa hiyo ni fursa kwa wawekezaji.
‘’Kama
bidhaa hizi zingekuwa zinatengenezwa hapa hapa nchini, zingekuwa zinapatikana
kwa bei nafuu na hivyo ingekuwa ahueni kwa wachimbaji wadogo kwasababu kwa hivi
sasa inabidi tuagize nje,’’ anasema Joyce.
Kampuni
ya MAPESSA ni ya mchimbaji, inauza vifaa mbalimbali zikiwemo compressor na
mashine za kuchenjua mawe ya madini ambazo zinaweza kutumiwa kwenye migodi
midogo na mikubwa ‘’Hapa kwetu mteja anaweza kuwekeza kidogo kidogo pindi
anapokamilisha malipo yote anakabidhiwa vifaa vyake,’’ anaeleza Joyce.
Joyce
ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kutumia mashine za kisasa badala ya njia za
asili kwani zinasaidia kuepusha ajali na kuongeza uzalishaji huku akitoa wito
kwa wanawake kutokuogopa kuingia katika sekta ya madini kupitia fursa
mbalimbali.
Akizungumzia
mchango wa madini kwenye biashara hiyo alisema mmiliki wa biashara hiyo ni
mchimbaji ambaye amewekeza katika uuzaji wa vifaa na kemikali akilenga
kurahisisha shughuli za madini. ‘’mtaji wa kuanzisha biashara hii aliupata
kupitia uchimbaji na hii imewezesha pia na sisi kupata ajira hapa,’’ anasema
Joyce.
Mapessa
Intertrade Ltd ilianzishwa rasmi 2023,
Itumbi Chunya kama kituo kidogo hadi
mwezi Juni 2025 ambapo makao makuu yake yalianzishwa Chunya mjini
ikilenga kuwasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kisasa kuendana na teknolojia za
kisasa kupitia bidhaa zinazouzwa na kampuni hiyo.
Kwa
mantiki hiyo, Mapessa Intertrade inatoa mfano hai wa namna shughuli za madini
zinavyoweza kuchochea biashara nyingine zinazosaidia maendeleo na uchumi wa
ndani. Ushiriki katika sekta ya madini hauishii kwenye uchimbaji pekee –
watanzania na wawekezaji wanaweza kushiriki katika hatua mbalimbali kama vile
uzalishaji wa vifaa, usambazaji wa kemikali, usafirishaji na hata huduma za
kitaalamu.
Serikali
tayari imeweka mazingira wezeshi, hivyo huu ni wakati muafaka kwa wadau mbalimbali
kuchangamkia fursa hii pana ya mnyororo wa madini ili kukuza ajira na mapato
ndani ya nchi.
Vision
2030: Madini ni Maisha na Utajiri
Madini ni
Ajira, Uchumi na Maendeleo



0 Maoni