Jamii imeaswa kuwapeleka watoto vituo vya kutolea huduma za
afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya Saratani za watoto.
Wito huo umetolewa na
Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya
Dkt. Ona Machangu wakati akitoa elimu ya afya kuhusu Saratani za Watoto kupitia
Mitandao ya Kijamii ya Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma.
Dkt. Machangu amesema ugunduzi wa mapema wa Saratani za
watoto husaidia matibabu ya mapema na kuweza kupona haraka.
“Saratani za Watoto sio hukumu na kifo,ugunduzi wa mapema
unasaidia kutibu tatizo hilo na nisisitize mara uonapo dalili mzazi, mlezi mchukue mtoto umpeleke katika
kituo cha kutolea huduma za afya ili aweze kufanyiwa uchunguzi,matibabu ya
haraka yanaweza kuchochea mtoto kupona,” amesema Dkt. Machangu.
Aidha, Dkt.Machangu ameainisha baadhi ya Saratani za Watoto
ni pamoja na homa za mara kwa mara, kikohozi kisichopona, kupungua uzito,
kupata uvimbe, michubuko kiurahisi, kudhoofika na kuishiwa nguvu, kushindwa
kutembea au kusimama vizuri, maumivu ya mifupa na viungo, upungufu wa
damu,mg’ao mweupe na hata kengeza machoni, au jicho kuvimba.
“Dalili za Saratani kwa watoto zinaweza kufanana na magonjwa
mengine kama homa, hivyo mtoto aonapo mojawapo ya dalili hizi usichukulie kama
ni tatizo dogo ni vizuri mchukue umpeleke katika kituo cha huduma za afya,” amesisitiza.
Halikadhalika, Dkt. Machangu ametaja baadhi ya aina ya
Saratani zinazoweza kuwapata watoto ikiwa ni pamoja na Saratani ya Damu,
Saratani ya Ubongo, Saratani ya jicho ambayo mara nyingi hugundulika kwa kuona
mng’ao mweupe kwenye jicho na si kila mng’ao mweupe ni Saratani.
Ikumbukwe kuwa, Saratani za Watoto ni kundi la magonjwa
ambapo inaweza kutokea pale seli za mwili zinakua na kuzaliana bila Mpangilio
na tofauti kati ya saratani ya watu wazima mara nyingi saratani za watoto
hazihusiani na mtindo wa maisha unaopelekea mtu kupata Saratani mfano uvutaji
wa sigara, ulaji usiofaa, au tabia bwete ambapo pia saratani za Watoto hutokea
kwa kasi.

0 Maoni