Mwenyekiti wa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele ametembelea na
kujionea maandalizi ya ujenzi wa vituo 83 kati ya 90 vya Wapiga Kura
vilivyotengwa maalum kwaajili ya wakazi wa zilizokuwa Kata za Ilangu, Ipwaga,
Bulamata na Mishamo zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi
ambazo zilifutwa na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa mujibu wa
Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura 287.
Jaji Mwambegele
alitembelea eneo hilo la Kata ya Tongwe katika Kitongoji cha Luhafwe jana Oktoba
26, 2025 akiwa ameambatana na Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Katavi, Msimamizi wa
Uchaguzi Jimbo la Tanganyika na watendaji wengine wa uchaguzi kuangalia
maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliopangwa kufanyika
Oktoba 29, 2025 nchini kote.
Akizungumza akiwa
katika eneo la Mnada wa Kitongoji cha Luhafwe, Jaji Mwambegele alisema Tume
ilitangaza kuhamisha baadhi ya vituo nje ya Makazi ya Wakimbizi hivyo amefika
na kuangalia maandalizi hayo na Tume imetoa matangazo katika maeneo yaliyofutwa
na imeweka vituo maeneo jirani.
Naye Msimamizi wa
Uchaguzi wa Jimbo la Tanganyika Bi.Kagemlo Mutagwaba amesema wapiga kura kutoka
kata zilizofutwa wamehamasishwa na wameonesha utayari wa kujitokeza kupiga Kura
katika maeneo mapya yaliyotengwa.
Watanzania wanataraji
kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 29, 2025
huku kauli mbiu ikiwa ni “Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura.



0 Maoni