WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameungana na viongozi wa nchi za India, China, Mauritius
na Comoro kwenye sherehe za kumuapisha Rais wa Jamhuri ya Shelisheli, Dkt.
Patrick Herminie zilizofanyika kwenye Uwanja wa Umoja, jijini Victoria nchini
humo.
Waziri
Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuwa miongoni mwa
viongozi hao wakuu wakiwemo Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na viongozi wa juu
kutoka vyama rafiki vya siasa. Rais Herminie aliapishwa jana (Jumapili, Oktoba
26, 2025) kuwa Rais wa sita wa nchi hiyo.
Viongozi
hao ni Makamu wa Rais wa India, Bw. Chandrapuram Ponnusamy Radhakrishnan;
Waziri Mkuu wa Mauritius, Dkt. Navinchandra Ramgoolam; Makamu wa Rais wa Chama
cha Chinese People’s Political Consultative Conference (CPPCC) Bw. Gao Yunlong
na Rais wa Baraza la Mawaziri la Kamisheni ya Bahari ya Hindi ambaye pia ni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Bw. Mohamed Mbae.
Mheshimiwa
Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Bw. Cosato Chumi; Balozi wa Tanzania nchini Kenya
anayeiwakilisha Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Bernard Kibesse na maafisa
waandamizi wa Serikali.
Ushindi
wa Rais Herminie, umekiondoa chama kilichokuwa madarakani cha Linyon Demokratik
Seselwa (LDS) ambacho kilishinda uchaguzi wa mwaka 2020. Rais Herminie ambaye
mwaka huu aligombea nafasi ya urais kupitia Chama cha United Seychelles (US)
aliapishwa jana baada ya kupata asilimia 52.7 ya kura zilizopigwa na kumshinda
mpinzani wake, Bw. Wavel Ramkalawan wa chama cha LDS aliyepata asilimia 47.3 ya
kura zote kwenye duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 11, 2025. Katika
duru ya kwanza iliyofanyika Septemba 27, mwaka huu hakuna mgombea urais
aliyezidi asilimia 50 ya kura zote baina ya wagombea sita wa urais.
Katika
sherehe hizo, Rais Dkt. Herminie alikula kiapo kwanza cha utii kwa wananchi
mnamo saa 12.35 jioni na kisha akala kiapo cha urais saa 12.37 na kutia saini
hati hizo mbele ya Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Rony Govinden.
Akilihutubia
Taifa hilo mara baada ya kuapishwa, Rais Dkt. Herminie alisema anakubali
kupokea dhamana aliyopewa na wananchi wa Shelisheli kwa kuwa anatambua wajibu
mkubwa unaotokana na Ilani ya chama chao isemayo: “Kwa ajili ya wengi, na siyo
wachache."
Rais
huyo alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi wake kuwa wasitarajie kuwa mambo
yote yatafanyika ndani ya siku moja. “Ninaongea kwa dhati kuwa mambo yote
hayawezi kukamilika ndani ya siku moja. Lakini kuanzia leo tutaanza kazi,
tutayapa kipaumbele masuala yote ya muhimu yanayogusa maisha ya wananchi na kwa
msingi huo, Serikali yangu imeanzisha “Siku 100 za Kwanza - Mkataba wa Kijamii
na Watu wa Shelisheli.”
Katika
hotuba yake iliyodumu kwa dakika 17, Rais Dkt. Herminie aliiomba jumuiya ya
kimataifa iungane na nchi hiyo kujenga urafiki na mshikamano. “Tunataka tushirikiane,
tukue pamoja, tufanye biashara kwa usawa, tunakaribisha uwekezaji na
ubadilishanaji wa maarifa ambao utanufaisha pande zote mbili,” alisisitiza.
Pia
Rais Herminie alisisitiza kwamba Serikali yake italibeba kwa dhati suala la
vijana na siyo kulizungumzia tu kwenye majukwaa. “Ninyi vijana siyo kwamba
mnapaswa kusubiri fursa zijazo, ninyi mpo hapa katikati yetu; ninyi ni viongozi
wa kesho. Ninawasihi vijana wa Kishelisheli mjikite kwenye masuala ya ubunifu,
sayansi, teknolojia na akili unde kama hamtaki kuachwa kwenye hii dunia
inayoenda kwa kasi. Tutaijenga nchi yetu kwa pamoja na hatutaacha vipaji vyenu
vipotee wala ndoto zenu zipepee zikiacha nchi yetu tupu,” alisisitiza.
Dkt.
Herminie aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Seychelles kuanzia mwaka 2007 hadi 2016
na kabla ya hapo, alikuwa kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni kuanzia
mwaka 1998 hadi 2003.
Kabla
ya kuondoka uwanjani, Rais Dkt. Herminie alishuhudia nyimbo mbalimbali,
mashairi na fashfash ya mafataki iliyodumu kwa
zaidi ya dakika 5.
Rais
wa Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Patrick Herminie akiapishwa kwenye sherehe zilizofanyika
Jumapili, Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Umoja, jijini Victoria nchini humo.
Rais wa Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Patrick Herminie akihutubia wananchi baada ya kuapishwa kwenye sherehe zilizofanyika Jumapili, Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Umoja, jijini Victoria nchini humo.



0 Maoni