Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimekanusha taarifa
zinazosambaa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na baadhi ya vyombo vya
habari ikihamasisha walimu kutoshiriki kwenye shughuli za Uchaguzi Mkuu, ambapo
baadhi ya walimu hutumika kama wasaidizi wa shughuli za uchaguzi kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni na taratibu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Chama kimetoa rai kwa walimu, wanachama wote
na wananchi wote kwa ujumla kupuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli wala
msingi wowote na zinalenga kuleta taharuki, uzushi na uchonganisi ambao
unapaswa kupingwa kwa nguvu zote ili kulinda umoja, amani na utulivu ambao ni
tunu ya taifa letu.
Pia CWT inapenda kuwahakikishia walimu, Serikali na
wananchi wote kwa ujumla kuwa kitaendelea kushirikiana na mamlaka husika
kuhakikisha kuwa tabia hii ya utoaji taarifa potofu inakomeshwa ili kulinda
misingi na madhumuni ya uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria na
kanuni za nchi.
Katika taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu Joseph
Misalaba, CWT imewataka walimu wote kuendelea na msimamo wa kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba,
2025 kwenda kupiga kura kwani ndio msimamo wa chama ambao ulikwisha tolewa na
Msemaji wa Chama (ambaye ni rais wa CWT).
Taarifa hiyo
ilisisitiza walimu na umma kwa ujumla kuwa mabalozi wazuri wa upendo,
amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo thabiti ya taifa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadae.
Aidha, Chama Cha Walimu Tanzania kimeishukuru
serikali kwa kuendelea kutatua kero mbalimbali za walimu kwa kushirikiana na
chama cha walimu Tanzania (CWT).



0 Maoni