Mgombea
wa urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim,
amesema wananchi wa maeneo mbalimbali ya vijijini na mijini wamechoshwa na hali
ya maisha magumu, ukosefu wa ajira na ubovu wa miundombinu, wakitaka mabadiliko
ya kweli ya uongozi.
Akihutubia
mkutano wa kampeni uliofanyika leo katika viwanja vya Mbagala Zakhem, jijini
Dar es Salaam, Mwalim amesema kila anakopita kwenye kampeni anakutana na kilio
cha wananchi wanaolalamikia umaskini uliokithiri.
“Kila
ninapopita, wananchi wananililia kuhusu maisha magumu, hali mbaya ya barabara,
huduma duni za afya na elimu. Wengi wao, hasa vijana, wanasema wamechoka na
mwaka huu wanataka msela wao akalie kiti cha Rais,” amesema Mwalim.
Mwalim
amesema taifa linahitaji mabadiliko ya kweli, akisisitiza kuwa ni wakati wa
kuipa nafasi CHAUMMA kuongoza nchi, huku akitoa wito kwa Chama cha Mapinduzi
(CCM) "kukaa pembeni" kupisha mabadiliko ya kiutawala.
“Tumechoka
na maisha magumu. Tumechoka na uonevu. Tunahitaji mabadiliko ya kweli. CCM ikae
pembeni,” amesema.
Mwalim
ambaye ameendelea na ziara ya kampeni katika mikoa mbalimbali, amesema CHAUMMA
iko tayari kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania wote, hasa
makundi ya vijana na wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisahaulika.
Kauli
zake zimekuja wakati vyama vya siasa nchini vikiendelea na kampeni kuelekea
Uchaguzi Mkuu, huku wananchi wakifuatilia kwa karibu mijadala ya kisera kutoka
kwa wagombea mbalimbali.

0 Maoni