Tume ya
Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini imekutana na wadau wa
sekta ya madini wakiwemo wachimbaji, wanunuzi na wathaminishaji wa madini, kwa
lengo la kupanga bei elekezi za madini ya vito, hatua inayolenga kuimarisha
uwiano wa faida, kuongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza
jijini Dodoma leo Oktoba 24, 2025, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini
CPA. Venance Kasiki, amesema kikao hicho kimefanyika kwa ajili ya kufanya
tathmini na kuweka bei mpya zitakazotumika kwa kipindi cha miezi mitatu, kwa
kuzingatia mwenendo wa soko la dunia na gharama halisi za uzalishaji.
“Kupitia
bei elekezi tunahakikisha wachimbaji, wanunuzi na Serikali wote wananufaika kwa
uwiano. Serikali itapata mapato yake kupitia Mrabaha na Ada ya Ukaguzi, huku
biashara ikiendelea kwa uwazi na ushindani wa haki,” amesema Kasiki.
Amesema
hatua hiyo itaimarisha uthabiti wa soko, kuzuia upotevu wa mapato, na kujenga
uaminifu kati ya wadau wa sekta ya madini ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa
pato la Taifa.
“Bei hizi
zitakuwa wazi na zitapatikana kupitia tovuti ya Tume ya Madini na Ofisi za
Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa. Tunataka wadau wote wapate taarifa sahihi ili
kuondoa mianya ya udanganyifu na kuongeza ufanisi wa biashara ya vito nchini,”
amesisitiza.
Aidha,
Kasiki amesema Tume itaendelea kukutana na wadau kila robo mwaka kwa ajili ya
kufanya mapitio ya bei, kujadili changamoto kuendana na mabadiliko ya
teknolojia katika uthaminishaji wa madini duniani.
Kwa
upande wake, Kulwa Mkalimoto, Katibu wa Vito kutoka Shirikisho la Wachimbaji
Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), ameeleza kuwa bei elekezi zilizopitishwa ni rafiki kwa wadau wote na
zitasaidia kuleta uwiano wa faida katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.
“Kikao kimeenda vizuri, bei zilizowekwa ni
rafiki na zinaleta usawa. Wachimbaji watanufaika, wanunuzi watanufaika, na
Serikali itakusanya mapato yake kupitia Mrabaha, Ada ya Ukaguzi, HIV Response
Levy na Ushuru wa Huduma unaokusanywa na halmashauri,” amesema Mkalimoto.
Kikao
hicho pia kimeshirikisha vyama mbalimbali vya wadau wa sekta ya madini ikiwemo
Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), FEMATA, Chama cha
Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), na Chama cha Mabroka Tanzania
(CHAMMATA).




0 Maoni