Kuelekea Uchaguzi Mkuu, Jeshi la Polisi limetoa onyo
kali kwa mtu yeyote atakayejaribu kuandaa maandamano au uchochezi wa kihalifu.
"Anayetaka kuandamana atakamatwa, ikiwamo
wahamasishaji kama wataonekana," msemaji alieleza. Aliongeza kuwa Polisi
inatambua wahamasishaji wengi, hata wale ambao 'kwa kawaida hujificha.'
Katika utekelezaji wa sheria, Polisi imesisitiza
kuwa mbinu za kiteknolojia zimeimarishwa. "Tunajua wametengeneza majina
bandia feki, lakini katika ulimwengu huu wa teknolojia huwezi kujificha,"
alisema.
Alifichua kuwa vifaa vya kielektroniki vinawasaidia
kuwafuatilia hata wale ambao wanadhani
wamejificha.
Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni Msemaji
Mkuu wa Jeshi la Polisi David Misime alisema kwamba ni muda tu ukidhani kwamba
unachoichea halafu hushiriki hatutakukamata unajidanganya ni muda tu.
Hata hivyo, Polisi ilisisitiza kuheshimu haki ya
kupiga kura. "Kama unaonekana unapita kwenda kupiga kura, na tunakujua ni
mmoja ya wachochezi tutakuacha upige kura," alisema na kuongeza,
"Tutakusubiri ukimaliza, ndipo tutakukamata. Si unakosa la jinai?"
Kauli hii inatoa taswira kwamba Polisi itaweka kipaumbele katika usalama wa
uchaguzi huku ikihakikisha sheria inafuatwa kwa wale wanaotenda makosa ya jinai
wanakamatwa.
Kuhusu utoaji wa taarifa, msemaji huyo alikanusha
madai ya waandishi wa habari kwamba hakuna kinachofanyika. "Kila mara
Polisi wanatoa taarifa kwa umma... yapo
mengi tunayofanya, waandishi naapaswa kukumbushia haya ambayo ni
mwendeleo" alisema, akisisitiza kwamba Polisi huhakikisha ufumbuzi wa mashauri tata na magumu unapatikana.
Aidha, Msemaji wa Polisi alihimiza jamii kuanzia
kwenye kiwango cha familia kushughulikia matatizo kabla hayajawa uhalifu.
"Tusitupiane mpira," alisema. "Tuanzie katika familia.
Wanaodhulumiana, wapenzi kuoneana wivu na ushirikina," aliongeza.

0 Maoni