Kundi la
watalii waliojipambanua kupanda na kushuka mlima Kilimanjaro kwa masaa 24
wakitokea katika mataifa mbalimbali barani Ulaya, kama “Inspire Challenge
Group” lilianza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro siku mbili (2) zilizopita
na kufanikiwa kufika kilele na kushuka kwa muda huo kupitia lango la Marangu,
huku washiriki wake wakipumua kwa kutumia pua pekee baada ya kuziba midomo yao.
Hii
inakuwa ni “challenge” ya kwanza na ya kipekee ya kuweka rekodi mpya ndani ya
Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro (KINAPA). Kama ilivyo kawaida watu wengi
wanapopanda milima wakati mwingi hutumia njia mbili katika upumuaji hasa
unapokuwa unahema kwa sababu ya kutembea kwa haraka au unapopanda sehemu
iliyoinuka.
Safari
hiyo ya kipekee imeanzia katika Hoteli ya Selig mjini Moshi ambako washiriki
hao walifanya mazoezi mepesi, yakiwemo yale yanayolenga kuimarisha upumuaji kwa
kutumia pua pekee.
Baada ya
maandalizi hayo, kundi hilo lilielekea langoni Marangu, ambako walipokea
maelekezo ya usalama, kufanya usajili rasmi, na kugawiwa viziba midomo kabla ya
kuanza kupanda mlima kuelekea Kilele cha Uhuru, ambacho ni sehemu ya juu kabisa
barani Afrika yenye urefu wa mita 5895 kutoka usawa wa bahari.
Safari
hiyo pia imekuwa kivutio kwa wadau wa utalii, wakiwemo viongozi wa KINAPA na
mashirika ya utalii, wanaoamini kuwa “challenge” hiyo itachochea utalii wa
ustahimilivu na kuongeza hamasa kwa watalii wengi kuja na “challenge” nyingine
tofauti ndani ya Mlima Kilimanjaro.
Safari
hiyo ya kuvutia na yenye mvuto wa aina ya kipekee imeratibiwa na kampuni ya
utalii ya Thomas Safaris & Treks Limited, ikihusisha jumla ya washiriki 13
kutoka nchi za Italia, Ufaransa, Uswisi na Ubelgiji, huku ikishirikisha timu ya
wasaidizi 30 wakiwemo waongoza watalii, wapishi na wabeba mizigo.
Na. Jacob
Kasiri - Kilimanjaro


0 Maoni