WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema kuwa madereva wa Serikali wanawajibu wa kufanya kazi
kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu ikiwemo ukaguzi wa gari kabla na baada ya
safari, kujaza na kutunza kikamilifu taarifa za safari na matengenezo.
Amewataka
madereva na wasimamizi wahakikishe usalama wa vyombo vya usafiri, abiria,
mizigo na nyaraka za Serikali pamoja na kutumia vifaa vya kisasa vya usalama,
na kujiepusha na tabia zinazoweza kuhatarisha maisha, mali na siri za Serikali.
Ameyasema
hayo leo (Jumanne, Septemba 2, 2025) alipofungua Mkutano wa Chama cha Madereva
wa Serikali Tanzania (CMST), jijini Dodoma. Amesema chama hicho kimekuwa nguzo
muhimu katika kuboresha huduma za udereva Serikalini na kuchangia maendeleo ya
Taifa kwa ujumla.
Pia, Waziri
Mkuu amewahakikishia madereva hao kuwa Serikali inaendelea kufanyia kazi
changamoto mbalimbali zinazowakabili madereva ili kuendelea kuimarisha
mazingira ya kazi na ustawi wa madereva wa Serikali kote nchini.
“Changamoto
mlizowasilisha ni mwendelezo wa kazi kubwa iliyopo mbele yetu, na kwa
ushirikiano kati ya Serikali, Waajiri na Chama cha Madereva, tutaendelea
kusonga mbele kwa hatua madhubuti ili kuboresha kada hii muhimu kwa manufaa ya
Taifa letu.”
Pia, Waziri
Mkuu amewataka waajiri wahakikishe stahiki za madereva zinalipwa kwa wakati,
mafunzo ya mara kwa mara yanafanyika, miundo ya ajira inatekelezwa ipasavyo na
wanapewa kipaumbele katika motisha mbalimbali.
Kwa upande
wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema madereva ni mhimili muhimu
katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Serikali na nidhamu na uadilifu
ndio msingi wa heshima wa kada hiyo.
“Sisi
Serikali tutahakikisha ustawi wa madereva unakuwa kipaumbele chetu, wao
wakiishi vizuri maana yake ni kwamba watafanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.”
Waziri Ulega
amesema lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto na kubadilisha uzoefu na
kuimarisha mshikamano.
Naye, Katibu
Mkuu wa CMST, Castro Nyabange amesema kuwa chama chicho kinampongeza kwa dhati
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua mbalimbali za kuboresha
maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo madereva.
“Upandishaji
wa mishahara kwa watumishi umetugusa pia sisi madereva, awali sisi madereva wa
Serikali tulikuwa na mishahara ya viwango vya chini sana, tunaahidi kufanya
kazi bega kwa bega na Serikali kwa kuzingatia weledi katika utendaji.”
Mkutanao huo
wenye kaulimbiu isemayo “Dereva wa Serikali, Epuka Ajali, Linda Gari Lako na
Watumiaji Wengine wa Barabara na Oktoba Shiriki Uchaguzi Mkuu”.
umehudhuriwa na madereva wa Serikali zaidi ya
2,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
0 Maoni