Chama cha
Mapinduzi (CCM) mkoani Geita leo Septemba 2, 2025 kimezindua kwa kishindo
kampeni za kuinadi Ilani ya CCM 2025-2030 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025
ambapo imeelezwa kuwa mpaka sasa tayari Majimbo 7 kati ya 9 ya Ubunge yamepita
bila kupingwa huku kata 92 kati ya 122 zikipita bila kupingwa.
Mgeni rasmi
katika uzinduzi huo uliofanyika katika Kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe, Mkoani
Geita ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa huo, Nicholaus
Kasendamila amesema Chama cha Mapinduzi kinaingia kwenye kampeni kikiwa na
mtaji mkubwa wa uadilifu, uaminifu, uchapakazi na busara ya mgombea Urais wa
kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema
kupitia kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, CCM inazo sababu za kuomba ridhaa ya
wananchi kuendelea kuongoza nchi akisema kuwa amefanya maendeleo mengi ikiwemo
uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kubwa la biashara
kwaTanzania na nchi jirani, amejenga daraja refu la Busisi, amekamilisha ujenzi
wa Bwawa la Julius Nyerere (MW 2,115) na reli ya kisasa imeshaanza kufanya
kazi.
Kasendamila
amesema kuwa katika Mkoa wa Geita, Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025
imetekelezwa kwa mafanikio ambapo ameeleza kuwa shule mpya za msingi 151
zimejengwa, Shule za sekondari mpya 118 zimejengwa, zimejengwa hospitali mbili
za rufaa, hospitali za wilaya mpya 4 na vituo vya afya 17 vipya vimejengwa.
Ameongeza
kuwa, kupitia Ilani ya CCM 2020-2025, zahanati 69 zimejengwa, leseni za madini
7600 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo na kuhusu umeme, kabla ya kuingia kwa
Serikali ya Awamu ya Sita kulikuwa na vijiji 362 tu vyenye umeme lakini sasa
vijiji vyote 486 mkoani Geita vina umeme.
Kuhusu
miundombinu ya Barabara amesema Barabara za lami na changarawe zimeendelea
kujengwa mkoani Geita ili kurahisisha usafiri wa wananchi.
Ametaja
vipaumbele vya CCM katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuwa ni pamoja na kuongeza
fursa za wananchi kujiimarisha kiuchumi, kuendeleza sekta mbalimbali ikiwemo
afya, elimu, madini, umeme n.k
Mwenyekiti
huyo wa CCM, ameomba wananchi waipigie kura CCM kwani kura zao zitafanyiwa kazi
kupitia maendeleo.
Akizungumza
kwa niaba ya Wagombea nafasi ya Ubunge mkoani Geita, Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye ni Mbunge Mteule wa Jimbo la
Bukombe, amewashukuru wananchi kwa
kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi wa kampeni akieleza kuwa ni ishara ya Wananchi kukipenda Chama cha
Mapinduzi na kuridhika na kazi zinazofanywa na Dkt. Samia suluhu Hassan.
Amesema
uchaguzi wa mwaka huu utapeleka salaam ndani ya nchi na kimataifa kuhusu uwepo
wa demokrasia nchini hivyo amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura
akiahidi kuwa maendeleo wanayoyaona sasa ni rasharasha tu kwani maendeleo
makubwa zaidi yanakuja.
Amesema Mkoa
wa Geita unazidi kukua ambapo kwa sasa umekuwa ni moja ya mikoa mitano yenye
uchumi mkubwa nchini ni mkoa namba moja kwa kuzalisha dhahabu, umekuwa ni mkoa
kiungo kwa maeneo mengine nchini na watu wake ni wachapakazi hivyo watampigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan ili
kupata maendeleo zaidi.
Kuelekea
uchaguzi Mkuu 2025, Dkt. Bitelo amesisitiza kuwa uchaguzi huo uunganishe
wananchi badala ya kutenganisha, kuwe na kampeni za kistaarab na Chama cha
Mapinduzi kuendelea kufanya kazi kwa umoja.
"Uchaguzi
huu ni kwa ajili ya maendeleo yetu, tunataka barabara bora, umeme, afya, mitaji
ya biashara, tusiuchukulie poa uchaguzi
huu kwani maana kubwa kwenye maisha yetu," Amesisitiza Dkt. Biteko
Akizungumzia
maendeleo mbalimbali yaliyofanywa katika Jimbo la Bukombe, Dkt. Biteko amesema,
chini ya uongozi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan Bukombe sasa kunajengwa Chuo cha
VETA ambacho kitawezesha vijana kupata ujuzi wa aina mbalimbali pia Chuo cha
Uhasibu Arusha kimeanzisha tawi wilayani Bukombe.
Ameongeza
kuwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezigusa sekta zote kimaendeleo akitolea mfano
Shule za msingi sasa zimefikia 104,
shule za sekondari zimefikia 25 na shule za sekondari kidato cha tano na
sita zimefikia 5 huku umeme ukifika kwenye vijiji vyote.
Ameongeza
kuwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha ujenzi wa kituo kikubwa cha kuzalisha
umeme wa jua wa megawati 5 wilayani Bukombe, kikiwa ni cha pili kwa ukubwa
ukiacha kituo cha namna hiyo kilichopo Kigoma pia anajenga barabara ya lami
kutoka Ushirombo hadi Katoro.
Katika hatua
nyingine Dkt. Biteko amewaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea mgombea
mwenza wa Kiti cha Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye
anatarajiwa kuanza ziara mkoani Geita tarehe 5 Septemba 2025.
Awali,
Katibu wa CCM Mkoa wa Geita, Alexandarina Katabi amesema Mkoa wa Geita una
mtaji wa wapiga kura waliojiandikisha takriban 1,532,408 huku Wanaccm waliojiandikisha
wakiwa ni 524,000 ikiwa ni mtaji wa nusu ya wananchi waliojiandikisha.
Amesema
katika Mkoa wa Geita, Majimbo yanayogombewa ni 9 na kata ni 122.
Ameongeza
kuwa katika Majimbo hayo 9 majimbo 7 tayari yamepita bila kupingwa na katika
kata 122 tayari kata 92 zimepita bila
kupingwa na zilizobaki ndizo zenye wapinzani.
0 Maoni