Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amekutana na kuzungumza na Mjumbe
Maalum wa Biashara wa Uingereza kwa Afrika Mashariki, Mhe. Kate Asamor
(Mbunge), katika Jumba la Commons, jijini London.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa
kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza, kupitia miradi
inayoendelea na mipango mipya inayohusisha nishati, madini, uchumi wa buluu,
fedha za kijani, ubunifu wa kidijitali na kilimo cha mazao ya biashara.
Waziri Kombo alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania
kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na kuhakikisha miradi
inayoungwa mkono na taasisi za kifedha za Uingereza, ikiwemo UK Export Finance
(UKEF) na British International Investment (BII), inatekelezwa kwa ufanisi.
“Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria na Uingereza
na inatambua mchango mkubwa wa miradi ya uwekezaji katika kuongeza ajira,
kukuza biashara ya kikanda na kimataifa, na kuendeleza sekta za kipaumbele kama
madini muhimu, nishati safi, na uchumi wa buluu,” alisema Mhe. Waziri Kombo.
Kwa upande wake, Mhe. Asamor aliipongeza Tanzania kwa hatua
inazochukua kuboresha mazingira ya uwekezaji na kusisitiza dhamira ya Uingereza
kuendelea kushirikiana kwa karibu katika miradi ya kimkakati. Alieleza kuwa
Uingereza iko tayari kusaidia upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kilimo,
kuimarisha miradi ya miundombinu ya Zanzibar na kusaidia miradi ya kijani na
kidijitali.
Mazungumzo hayo pia yaligusia maandalizi ya uchaguzi mkuu wa
Tanzania unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ambapo Waziri Kombo
alibainisha kuwa kwa mara ya kwanza uchaguzi huo unasimamiwa na tume huru ya
uchaguzi, hatua ambayo itaongeza uwazi na kuimarisha imani ya wawekezaji.
Pande zote mbili zilithibitisha kuendeleza uratibu wa karibu kupitia Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority (TISEZA) na kukubaliana kuanzisha timu ya ufuatiliaji (delivery team) ya pamoja itakayokuwa na mapitio ya robo mwaka ili kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa makubaliano yaliyofikiwa.




0 Maoni