Mgombea wa Ubunge Jimbo la Bukombe, Ndugu Doto Mashaka Biteko amewahimiza wananchi wa Kata
ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani Geita kujitokeza kwa wingi na kuwapigia kura
wagombea wa CCM ili kukipatia chama hicho ushindi wa kishindo katika Uchaguzi
Mkuu ujao Oktoba 29, mwaka huu.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 9, 2025 wakati akiendelea
na kampeni katika Kata ya Busonzo wilayani Bukombe mkoani humo.
Amesema eneo la Idoselo katika Kata ya Busonzo lilikuwa na
changamoto kadhaa ikiwemo barabara na shule.
Kufuatia hali hiyo, Rais Samia alielekeza wananchi wa eneo
hilo wachongewe barabara, wajengewe shule na hospitali.
“ Hapa Idoselo tumejenga Kituo Kikubwa cha Kuzalisha umeme
megawati 5 ili wananchi waweze kupata umeme, tunataka kuongeza upatikanaji wa
maji na baada ya uchaguzi tutapanua chanzo cha maji ili kuhakikisha kunakuwa na
maji ya uhakika,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja vipaumbele vya CCM ni kujenga shule nyingine ya
sekondari Idoselo ili kupunguza adha ya
wanafunzi kwenda kusoma Busonzo.
Aidha, amewahimizi wananchi na wajumbe wa CCM kujitokeza kwa
wingi kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu na kumchagua mgombea wa Urais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan ambapo pia amewaomba wananchi wamchague kwa nafasi ya Ubunge wa
Bukombe pamoja na mgombea Udiwani Merikiori wa Busonzo.
Akimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Busonzo, amesema mgombea
huyo ni mchapakazi na anayetaka maendeleo hivyo, wananchi wamchague ifikapo
Oktoba 29 huku akisisitiza kuwa ili CCM ishinde kwa kishindo wananchi
wajitokeze kwa wingi kupiga kura.
Naye, Mgombea wa nafasi ya Udiwani Kata ya Busonzo, John Merikiori amesema ni
wajibu wa wananchi kupiga kura na kuchagua wagombea wa CCM ambao wakipata
dhamana ya uongozi watahakikisha wanaleta maendeleo kwa wananchi.
0 Maoni