Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewaua watu wawili wanaodaiwa kuwa sehemu ya
genge lililomhusisha na utekaji na mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa
Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Mbeya, marehemu Shyrose Michael Mabula (21).
Tukio
hilo limekuja wiki mbili baada ya mwili wa marehemu Shyrose kupatikana Septemba
16, 2025 majira ya saa 5:00 usiku katika Mtaa wa Morovian, Kata ya Isyesye
jijini Mbeya, ukiwa umechomwa moto. Taarifa za awali zilieleza kuwa marehemu
alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana Septemba 14, 2025.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga uchunguzi wa awali
ulioanzishwa mara baada ya tukio hilo uliwawezesha maofisa wa upelelezi kumtia
nguvuni Marwa Nyahega John (25),
mkazi wa Uzunguni “A” Mbeya, aliyekiri kuhusika kwenye utekaji huo pamoja na
wenzake wawili Edward Christopher
Kayuni na Websta William
Mwantebele.
Kamanda Kuzaga
alisema kuwa watuhumiwa hao walimteka Shyrose kwa lengo la kumtumia kama chambo
cha kupata kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa baba yake mzazi, Dkt. Michael Mabula. Baada ya
kushindwa kufanikisha mpango huo, walimuua kwa kumlazimisha kunywa sumu ya
kuulia magugu aina ya Round Up,
kisha walimnyonga na baadaye kuchoma mwili wake ili kuficha ushahidi.
Mauaji Wakiwa Mikononi mwa Polisi
Taarifa
ya Polisi inaeleza kuwa tarehe 25 Septemba, 2025, mtuhumiwa Websta William Mwantebele (27),
ambaye ni mlinzi, alikamatwa na kuhojiwa, ambapo alikiri kushiriki katika
utekaji na kuua binti huyo. Pia alieleza kuwa walikuwa wamepanga kukutana na
wenzake waliobaki katika eneo la machimbo, Kijiji cha Chalangwa, Wilaya ya
Chunya.
Mnamo
Septemba 27, 2025, Mwantebele aliwaongoza askari hadi eneo hilo kwa ajili ya
kuwaonyesha wenzake. Askari walijipanga na kuweka mtego, ambapo muda mfupi
baadaye alifika mtu aliyedaiwa kuwa ni Edward
Christopher Kayuni.
Alipoelezwa
kuwa anakamatwa, alitoa kisu ghafla na kujaribu kuwashambulia askari. Hata
baada ya onyo la mara kadhaa na risasi za hewani, mtuhumiwa alikaidi na ndipo
alipopigwa risasi mguuni na kuanguka.
Wakati
purukushani hiyo ikiendelea, mtuhumiwa Websta William Mwantebele naye
alijaribu kukimbia kuelekea kichakani, lakini alipigwa risasi mguuni na
mgongoni baada ya kushindwa kusimama licha ya onyo. Watuhumiwa wote wawili
walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya, lakini walithibitishwa
kufariki dunia mara baada ya kufikishwa hospitalini.
Ushirikiano na Mganga wa Jadi
Katika
hatua nyingine ya uchunguzi, mtuhumiwa Marwa
Nyahega John alieleza kuwa baada ya mauaji, alimkata marehemu kidole cha
mkono wa kushoto na pamoja na nguo zake za ndani, alizipeleka kwa mganga wa
jadi maeneo ya Isyesye kwa ajili ya kufanya “zindiko” ili wasibainike na
kukamatwa na Polisi.
Akiwa
njiani kuwaongoza askari hadi kwa mganga huyo, Marwa aliruka ghafla kutoka
ndani ya gari la Polisi na kujeruhiwa vibaya kichwani. Alikimbizwa Hospitali ya
Rufaa Kanda ya Mbeya ambako alithibitishwa kufariki dunia.
Katika
upekuzi uliofanywa kwenye maficho ya watuhumiwa, Polisi walikuta pingili mbili
za vidole, vitambulisho bandia viwili vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
vilivyo na majina na picha za watuhumiwa hao, pamoja na simu mbili zilizokuwa
na picha na taarifa mbalimbali zinazoonyesha mawasiliano na ushahidi wa
utekaji.
Jeshi la Polisi Latoa Rai
Akizungumza
na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kuzaga alitoa wito kwa
vijana waliopitia mafunzo ya kijeshi au ya kiusalama kutumia ujuzi huo kwa
mujibu wa sheria na si kwa kutenda vitendo vya kihalifu.
Aidha,
alitoa tahadhari kwa wananchi kuacha tamaa ya kutaka utajiri wa haraka kwa njia
za uhalifu, akisisitiza kuwa sheria haitamwacha yeyote atakayehusika na vitendo
vya utekaji, mauaji au ushirikiano na magenge ya kihalifu.
"Tunaendelea na msako wa kuwatafuta washirika
wengine wa genge hili, ikiwemo mganga wa jadi aliyepokea viungo vya marehemu.
Hatutapumzika mpaka wote waliohusika wakamatwe na kufikishwa mbele ya
sheria," alisema
Kamanda Kuzaga huyo.


0 Maoni