Mgombea
urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
amewataka wakazi wa Mkoa wa Tanga kukaa 'mkao wa kula' kutokana na mipango ya
miradi ya maendeleo itakayoufungua mkoa huo.
Amesema
akipewa tena ridhaa ya kuiongoza serikali ijayo ya Tanzania, atairejesha Tanga
ya viwanda kwani viwanda ni moja ya kipaumbele cha serikali katika miaka mitano
ijayo.
Dkt.
Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 29, 2025 kwenye Viwanja vya
Usagara jijini Tanga alipohutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni.
"Wana
Tanga mkae mkao wa kula. Tunataka kuirejesha ile Tanga ya viwanda," alisema.
Amesema
tayari Tanga imekuwa na mafanikio na maendeleo makubwa kutokana na maboresho ya
Bandari ya Tanga ambayo itakuwa na bohari ya mafuta na gesi.
Kutokana
na maboresho hayo, bandari hiyo itaongeza ajira 2,100 kwa wana Tanga na
kunyanyua uchumi wa wananchi wake.
Aidha,
amesema Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefikia
asilimia 84 na umetoa ajira 1,300 kwa wakazi wa Chongoleani na jumla ya ajira
2,000 ndani ya Tanga.
Akizungumza
mambo mazuri yajayo kwa wana Tanga, Dkt. Samia amesema serikali itajenga reli
ya Tanga - Arusha - Musoma ya kilometa 1,108 ambayo itaongeza fursa za ajira na
kukuza uchumi.
Amesema
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na Wakala ya
Barabara Tanzania (TANROADS) watajenga Barabara ya Handeni - Singida.
Ameutaja
mkakati mwingine kuwa ni kuipanua Barabara ya Dar es Salaam - Chalinze - Segera
kwa nia ya kupunguza msongamano wakati Mkoa wa Tanga ukifunguka kiuchumi.
Katika
kuirejesha Tanga ya viwanda, Dkt. Samia amesema kutajengwa Kiwanda cha Chai
Korogwe, huku Kiwanda cha Foma kikiwa kimeshafufuliwa,na Kiwanda cha Saruji
Tanga kimepanuliwa na kuongeza uzalishaji na kunajengwa kiwanda cha kuunganisha
magari ya kubeba wagonjwa(ambulance).
"Haya
yote yanaongeza uwekezaji, hivyo maeneo yaliyokamatwa na watu ambayo
hayajaendelezwa yatwaliwe na kupewa wawekezaji," amesema Dkt. Samia.
Amebainisha
kuwa kutajengwa viwanda viwili vya sukari, kimoja katika Bonde la Pangani kwa
sukari ya majumbani na kingine Tanga kwa sukari ya viwandani.
Pia
katika bonde hilo kutakuwa na skimu ya umwagiliaji itakayotoa ajira 20,000 itakayojengwa
kwa gharama ya Shilingi bilioni 87.
Amewaahidi
machinga kuwa serikali yake ijayo itawajengea soko lenye uwezo wa kuwahudumia
wafanyabiashara 1,400 kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.9,
pamoja na
ujenzi wa kiwanda cha dawa na vifaa tiba.
Akiwa
Pangani, ameahidi kukamilisha Daraja la Pangani na Barabara ya Tanga - Pangani -
Makurunge, pamoja na ujenzi wa soko la kimataifa la samaki Kipumbwi.
Akiwa
Muheza, mbali ya kuahidi kujenga na kukamilisha barabara za Muheza - Pangani
kilometa 45 na Muheza - Amani kilometa 40,mgombea huyo wa Urais wa CCM ameahidi
serikali ijayo itajenga kongani za viwanda vya matunda na viungo.
Aboubakary
Liongo - Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na
Mafunzo CCM


0 Maoni