Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa salamu za pongezi kwa Jamhuri ya Watu
wa China (PRC) kwa kuadhimisha miaka 76 tangu kuanzishwa kwa taifa hilo, ambalo
kwa sasa lina nafasi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani.
Salamu
hizo ziliwasilishwa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, katika
hafla maalumu ya maadhimisho iliyofanyika Septemba 29, 2025 katika makazi ya
Balozi wa China jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo, Waziri Kombo aliipongeza China kwa hatua kubwa ilizopiga
katika nyanja za maendeleo ya kiuchumi, sayansi na teknolojia ndani ya kipindi
cha miaka 76 tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa taifa hilo ni mfano wa
kuigwa duniani na mshirika muhimu kwa maendeleo ya Afrika, hasa Tanzania.
“Uhusiano
kati ya Tanzania na China ni wa kihistoria, uliosimikwa katika misingi ya
urafiki, uwazi, usawa na kuheshimiana. Tunafarijika kuona uhusiano huu ukizidi
kuimarika kupitia ushirikiano katika maeneo mbalimbali kama biashara,
uwekezaji, elimu, afya, kilimo, utalii na miundombinu,” alisema Mhe. Kombo.
Aidha,
Waziri Kombo alieleza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana kwa karibu
zaidi na China katika kusaka fursa mpya za maendeleo na kuhakikisha misingi
iliyoweka uhusiano huo inadumishwa, akibainisha kuwa msingi huo ndiyo dira ya
uhusiano imara uliodumu kwa karibu miongo sita.
Kwa
upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen
Mingjian, alisema licha ya changamoto za kisiasa na kiuchumi zinazolikumba
dunia kwa sasa, China imeendelea kusimama imara katika kulinda ustawi wa
wananchi wake na kuchangia maendeleo ya dunia.
Balozi
Chen alibainisha kuwa China itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa
katika kusukuma mbele ajenda muhimu za maendeleo kama vile mabadiliko ya
tabianchi, usuluhishi wa migogoro, na kukuza usawa duniani kupitia programu na
majukwaa kama Belt and Road Initiative pamoja na Jukwaa la Ushirikiano wa China
na Afrika (FOCAC).
Katika
salamu zake, Balozi huyo pia aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza
uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo mbili, akisisitiza kuwa
uhusiano huo umejengwa katika misingi ya kuheshimiana, mshikamano na maendeleo
ya pamoja.
Hafla
hiyo ya maadhimisho ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali,
wawakilishi wa vyama vya siasa, mabalozi na wanadiplomasia kutoka mataifa
mbalimbali, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.





0 Maoni