Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania ni
miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika
matumizi ya rasilimali za ndani na kuwekeza katika sekta ya elimu kwa
maendeleo endelevu.
Amesema
hayo Septemba 24, 2025 jijini Dar es salaam wakati akifungua Kongamano la Tano
la Kimataifa la Elimu Bora lililoongozwa na kauli mbiu inayosema “Kuimarisha
mifumo na uwekezaji: Kusonga mbele katika Uhamasishaji wa Rasilimali za Ndani
kwa ajili ya Elimu Jumuishi, Bora na Endelevu Barani Afrika”.
Dkt.
Biteko ametaja hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwa ni pamoja na kutunga na
kuboresha Sera, Sheria na miongozo mbalimbali ya elimu, kuongeza kiwango cha
bajeti ya elimu kutoka shilingi za trilioni 4.72 kwa mwaka wa fedha 2020/2021
hadi kufikia shilingi za trilioni 6.16
mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema
ongezeko hilo la bajeti limeboresha mazingira na miundombinu mbalimbali ya
elimu kwa maendeleo endelevu. Vile vile, Serikali imetanua wigo wa Sera ya
Elimu bila malipo kwa elimu ya Sekondari ambapo mwaka 2020 kilitengwa kiasi cha
shilingi za Kitanzania bilioni 312.08 na mwaka 2024 kilitengwa kiasi cha
shilingi za Kitanzania bilioni 796.58 ikiwa ni sawa na ongezeko la shilingi
bilioni 484.
“Ongezeko
hili limeweza kupunguza changamoto za kifedha zinazorudisha nyuma sekta ya
elimu na hivyo kuongeza idadi ya wanufaika wa elimu malipo kutoka wanafunzi
14,940,925 wa mwaka 2020 hadi kufikia wanufaika 16,155,282 wa mwaka 2024,”
amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza
“Pamoja na mafanikio haya, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto nyingine kadhaa
katika sekta ya elimu kwa maendeleo endelevu.”
Amewahimiza
wadau wa kongamano hilo kuifanyia kazi kauli mbiu ya mwaka huu ili kufikia
utekelezaji wa matakwa ya kimataifa ya kutenga na kuelekeza asilimia 20 ya
bajeti ya nchi katika maendeleo ya sekta ya elimu.
Aidha,
amesema Afrika ikiwekeza katika elimu bora itaweza kutatua changamoto ya uhaba
wa walimu bora hususan maeneo ya vijijini. Ambapo, hadi kufikia mwaka 2030 Bara
hilo linahitaji kuwa na walimu milioni 17 ili kuwa na elimu bora ya msingi na sekondari na kuwa na mifumo thabiti
ya elimu ya kidigitali ambayo itasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo
nakuendana na mazingira tuliyonayo.
Ambapo
tafiti za Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) mwaka 2025
zinaonesha kwamba, elimu bora, kwa wastani, huchangia asilimia 20 hadi asilimia
30 ya ukuaji wa uchumi wa muda mrefu wa Taifa lolote. Tafiti hizo hizo pia
zinaonesha kuwa, mtu mwenye elimu ya juu hupata kipato kwa wastani wa asilimia
50 hadi asilimia 100 zaidi ya mtu asiyekuwa na elimu hiyo ya juu.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo amesema suala
la kugema raslimali fedha na watu vinaweza kuongeza ubora wa elimu na kupunguza
changamoto za sekta ya hiyo kwa kushirikiana na wadau.
Naye,
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema
kuwa Kongamano hilo linalenga kuboresha sekta ya elimu nchini na kuwa Wizara
yake ina jukumu la kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa katika viwango vya
kimataifa.
“
Kongamano hili limekuja katika wakati muafaka ambapo Serikali inaendelea
kuwekeza raslimali fedha, hivyo mkutano huo utasaidia kugema raslimali fedha
ili kuleta mabadiliko katika mfumo wa elimu,” amesema Prof. Nombo.
Meneja wa
Kanda wa Global Partnership for Education (GPE), Belay Addise amesema kuwa
Taasisi hiyo inajivunia ushirikiano wake mzuri uliopo kati yake na Serikali ya
Tanzania tangu mwaka 2013. Ambapo kupitia ushirikiano huo Tanzania imepokea
takribani dola za Marekani milioni 348 kupitia mashirika mbalimbali ikiwemo
UNICEF, UNESCO na Swedish Development Agency (SIDA) kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya elimu.
Mratibu
wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Martha Makala ameishukuru Serikali kupitia Wizara
ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na wadau wa elimu kutoka ndani na nje
nchi kwa kuwezesha Kongamani hilo na kuwa uwepo wa watunga sera katika
Kongamano hilo utasaidia kufanya mijadala kuwa yenye tija itakayoleta matokeo
chanya katika sekta ya elimu.
Na. Ofisi
ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni