Kwa muda
mrefu Wachimbaji Wadogo wamekuwa wakichimba kwa kubahatisha, mara nyingine wakipoteza
mitaji yao yote kwa sababu ya kukosa taarifa za uhakika kuhusu maeneo yenye
rasilimali. Lakini Serikali sikivu imeleta suluhisho la kudumu.
Taasisi
ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kuleta mageuzi
kwenye Sekta ya Madini kupitia huduma za utafiti wa madini kwa teknolojia ya
kisasa, zikiwa na gharama nafuu inayowalenga hasa kundi la Wachimbaji Wadogo.
Lengo likiwa kuondoa uchimbaji wa kubahatisha na kuhakikisha kila shilingi
inayowekezwa inaleta matokeo.
Akizungumza
mapema leo Septemba 24, 2025, Mfizikia Mkuu wa GST, Octavian Minja
amewasisitizia wachimbaji wadogo wanaotembelea banda la GST katika Maonesho ya
Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Viwanja vya Dkt. Samia
Suluhu Hassan, Bombambili – Geita, kuwa ni muhimu kufanya tafiti za jiosayansi
kabla ya kuanza uchimbaji ili kuongeza uzalishaji na kuepuka hasara.
“Wachimbaji
wadogo wanapaswa kuchangamkia fursa hii. Kupitia huduma zetu, wanaweza kupata
taarifa za kitaalamu kabla ya kuwekeza mitaji yao. Hii itapunguza hasara na
kuongeza tija,” anasisitiza Minja.
Anabainisha
kuwa wachimbaji wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na taarifa sahihi
za jiosayansi zinazoonesha miamba, madini na mwelekeo wa miamba husika, hali
inayowasababisha kuchimba kwa kubahatisha na kupoteza mitaji.
Kwa
mujibu wa Minja, GST inatumia vifaa vya kisasa vya jiofizikia vinavyoweza
kubainisha aina ya miamba iliyopo chini ya ardhi na mwelekeo wa miamba
iliyobeba madini. “Tunawaalika wachimbaji wote nchini kuitumia GST hususan katika
hatua ya utafutaji ili kuepuka kupoteza mitaji na uharibifu wa mazingira
unaosababishwa na uchimbaji holela,” anasisitiza Minja.
Huduma
hizi zimeletwa mahsusi kuendana na uwezo wa kifedha wa wachimbaji wadogo, huku
zikitoa matokeo sahihi na ya haraka. Tayari wachimbaji waliotembelea banda la
GST wameonesha shauku kubwa, wakieleza kuwa hii ndiyo fursa waliyoisubiri kwa
muda mrefu.
Kwa
maneno mengine, GST imekuwa daraja kati ya teknolojia ya utafiti na mchimbaji mdogo. Matokeo yake ni uchimbaji
wa uhakika, mitaji salama, na uchimbaji wenye tija.



0 Maoni