Mgombea
ubunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani
Kikwete, ameendelea na mikutano yake ya kampeni kwa kishindo, ambapo ameshiriki
kwenye uzinduzi wa kampeni za kunadi na kuomba kura kwa wagombea wa nafasi za
Udiwani, Ubunge na Urais kwa tiketi ya CCM. Mkutano huo mkubwa umefanyika
katika Kijiji cha Mihuga, Kata ya Miono, ndani ya Halmashauri ya Chalinze.
Akiongea mbele
ya wakazi wa kijiji hicho, Ridhiwani Kikwete aliwataka wananchi kuendelea kuiamini
CCM na kumuunga mkono kwa dhati mgombea urais wa chama hicho, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, akisisitiza kuwa rekodi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi
kilichopita ni ushahidi tosha wa uongozi bora.
“Tumeshuhudia
maendeleo makubwa katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
kuanzia miundombinu, elimu, afya, maji, hadi nishati. Haya yote yamewezekana
kwa sababu ya uongozi imara wa CCM unaofanya kazi kwa kushirikiana,” alisema
Ridhiwani huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria.
Aidha,
Ridhiwani aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchagua viongozi wote wanaotokana
na CCM kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge hadi Urais maarufu kama "mafiga
matatu".
Ameeleza kuwa
mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Ilani yanatokana na mshikamano na ushirikiano
kati ya viongozi hao, jambo linalowezesha serikali kutekeleza miradi ya
maendeleo kwa ufanisi.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM wa ngazi ya wilaya na mkoa,
pamoja na wapenzi na wanachama wa chama hicho waliokuja kuonesha mshikamano na
kuunga mkono kampeni za chama chao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.




0 Maoni