Katika
ulimwengu wa uchimbaji mdogo, changamoto kubwa imekuwa namna ya kupata dhahabu
kwa ufanisi na gharama nafuu, bila kupoteza rasilimali nyingi wala uharibifu wa
mazingira na ukitumia vifaa vya kawaida na nishati kidogo kulinganisha na CIP
zilizozoeleka.
Miaka kadhaa
iliyopita, wachimbaji wadogo walihangaika, dhahabu nyingi ilibaki kwenye
udongo, gharama za uchenjuaji zikiwa kubwa, na uharibifu wa mazingira
ulionekana kutokana na njia za kijadi za kuchejulia dhahabu.
Lakini
sasa, simulizi ya ubunifu wa mtambo wa uchenjuaji madini ya dhahabu (CIP)
inayotengenezwa kwa gharama nafuu ni teknolojia inayochenjua dhahabu kwa zaidi
ya asilimia 98%. Mtambo huo ambao umetengezwa tofauti kidogo na ile
iliyozoeleka umekuwa mkombozi wa wachimbaji wadogo.
Unapowekwa
udongo wenye dhahabu ndani yake, dhahabu inatoka kwa usahihi, ufanisi, na
kinachobaki ni udongo usio na madhara makubwa kwa mazingira.
John
Ngeda, ni mmoja wa wabunifu wa mtambo huo, anasema kuwa, safari yake ya maarifa
ilimpeleka nchini Zimbabwe, ambako alijifunza mbinu za uchenjuaji, kisha
akaamua kurudi nyumbani na kuboresha teknolojia hiyo kwa manufaa ya wachimbaji
wa Tanzania.
Matokeo
yake yamekuwa makubwa kwani zaidi ya mitambo 25 imejengwa katika Kanda ya Ziwa
pekee, na sasa ipo hadi Mbeya na Mpanda.
Wachimbaji
wadogo wanaona utofauti si tu kwamba wanapata dhahabu zaidi, bali pia wanaokoa
gharama kubwa walizokuwa wakitumia kwa njia zisizo na tija. Mazingira pia
yanapumua, kwa sababu teknolojia hii ni rafiki wa mazingira, ikipunguza madhara
yaliyokuwa yakisababishwa na kemikali hatarishi.
Katika
Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini Geita tarehe 23 Septemba 2025,
mtambo wa CIP umegeuka kivutio kikuu. Wananchi wanapata kushuhudia jinsi
teknolojia hiyo ilivyobadilisha maisha ya wachimbaji wadogo kutoka hali ya
kuchimba kwa mazoea na hatimaye kuchimba kwa tija zaidi.
Hii siyo
tu simulizi ya dhahabu, bali ni simulizi ya ubunifu wa Mtanzania, na ushindi wa
teknolojia rafiki kwa binadamu na mazingira.
Dhahabu
sio ndoto au madini yanayoambatana na ushirikina bali ni urithi unaleta
maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi pia huku ikibadili maisha ya maelfu.
Dhahabu
haipo tu ardhini; ipo pia kwenye mawazo ya wabunifu wanaothubutu.
0 Maoni