Rais Samia awaahidi neema zaidi wakulima wa tumbaku Tabora

 

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Taifa wa chama, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaahidi wakulima wa tumbaku nchini kuwa serikali yake takayoiunda itasimama nao bega kwa bega.

Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo alipohutubia mikutano ya kampeni za Uchaguzi Mkuu katika wilaya za Uyui, Urambo na Kaliua mkoani Tabora jana Alhamisi Septemba 11, 2025.

Amesema kwa sasa zao la tumbaku limekuwa na bei nzuri kimataifa na uzalishaji umeongezeka katika mkoa huo.

Amesema kutokana na hilo serikali yake imeongeza kampuni za ununuzi wa tumbaku ili kuongeza ushindani wa bei katika zao hilo.

Aidha, amewahakikishia wakulima hao wa tumbaku kuwa watalipwa madai yao ya fedha kwakuwa serikali iko katika mazungumzo na kampuni za PCL na Volecel ambazo hazijawalipa wakulima.

Hata hivyo, mgombea huyo wa Urais wa CCM amewataka wakulima hao kutokata miti kwa ajili ya kukaushia tumbaku badala yake watumie teknolojia za kisasa ili kulinda na kuhifadhi mazingira.

Dkt. Samia amesema juhudi zilizofanywa na serikali yake zimechangia kukua kwa uzalishaji wa zao la tumbaku kutoka tani 11, 208 mwaka 2021 hadi kufikia tani 20,494 huku ikifufua kiwanda cha tumbaku mkoani Morogoro ambacho kinaongeza thamani kabla ya kusafirisha nje.

"Niwahakikishie kwamba fedha hizo zitalipwa, kupitia Waziri wa Kilimo huwa ninataka ripoti kila baada ya muda aniambie mazungumzo yamefikia wapi ili wakulima walipwe fedha zao," alieleza Dkt. Samia.

Amewapongeza wakulima hao wa tumbaku wa Mkoa wa Tabora kwa kuongeza uzalishaji kutokana na serikali kutoa ruzuku ya mbolea.

Pia mapato ya wakulima yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 11 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 50 kwa mwaka 2024/25 huku bei ya tumbaku ikipanda kutoka dola moja kwa tani hadi sasa dola 2.5 kwa tani.

"Niwahakikishie tukipewa ridhaa tutafanya kila linalowezekana kulitengeneza zao la tumbaku na kutafuta masoko mazuri zaidi. Wito wangu kwa wana Tabora kupunguza kukata miti, tunakwenda kwenye teknolojia mpya ya kukausha tumbaku ili Urambo na Tabora yetu itunze mazingira yake yatakayosaidia kuwa mvua za kutosha na kupata maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo na shughuli zingine," alisema Dkt. Samia.

Leo Ijumaa Septemba 12, 2025 mgombea huyo wa CCM anatarajiwa kufanya mkutano mkubwa kwenye Viwanja vya Nanenane Ipuli mjini Tabora, kabla ya kuanza kampeni zake mkoani Kigoma kesho Jumamosi Septemba 13, 2025.

Na. Aboubakary Liongo - Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM

Chapisha Maoni

0 Maoni