TAWIRI yapinga ripoti mpya ya idadi ya nyumbu, yasema takwimu si sahihi

 

Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imepinga ripoti mpya ya utafiti iliyoandikwa na Isla Duporge na wenzake kuhusu idadi ya nyumbu katika mfumo wa ikolojia wa Serengeti-Mara, ikisema takwimu zilizotolewa si sahihi na haziwezi kulinganishwa na zile za taasisi hiyo.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Mkurugenzi wa Utafiti wa TAWIRI, Dkt. Julius Keyyu, taasisi hiyo imesema imepitia kwa kina chapisho hilo lililotolewa kwenye jarida la PNAS Nexus tarehe 9 Septemba 2025, ambapo waandishi wa ripoti hiyo walikadiria nyumbu kuwa 600,000 pekee, idadi ambayo TAWIRI imeielezea kuwa ni ndogo kupita kiasi na isiyoakisi uhalisia.

"Kulingana na sensa yetu ya hivi karibuni, nyumbu wanaokadiriwa kuwepo ni 1,366,109 (SE 231,741), kwa kutumia mbinu ya uhakika ya kupiga picha kwa ndege, ambayo imetumika kwa miaka mingi nchini Tanzania na hata kimataifa,” alisema Dkt. Keyyu.

Mapungufu ya Mbinu Mpya

Ripoti ya Duporge et al. ilitegemea teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence) kwa kutumia picha za setilaiti zenye uangavu wa kati ya sentimita 33 hadi 60. TAWIRI inasema mbinu hiyo bado ni mpya, haijahakikiwa (not validated), na haijawahi kutumika kwa mafanikio katika kuhesabu wanyamapori wengi kama nyumbu, hasa katika mazingira magumu ya miti na vichaka.

Kwa upande mwingine, TAWIRI hutumia mbinu ya kupiga picha kwa ndege kwa kutumia kamera zenye uangavu wa juu wa sentimita 3 hadi 5, ikijulikana kama Aerial Point Sampling (APS), ambayo imethibitishwa kisayansi na kuonyesha uwezo mkubwa wa kuona, kutambua, na kutofautisha nyumbu na wanyamapori wengine.

Wakati wa Sensa Watofautiana

Tofauti nyingine kubwa ni wakati wa utafiti. Sensa ya TAWIRI hufanyika kipindi cha masika (Februari-Machi), wakati nyumbu wote wanakusanyika kwenye nyanda za nyasi fupi za Serengeti Kusini, kaskazini mwa Ngorongoro na Loliondo, maeneo ambayo huwafanya kuwa rahisi kuonekana na kuhesabiwa kwa usahihi.

Kinyume chake, utafiti wa Duporge ulifanyika kipindi cha kiangazi (Agosti 2022 na 2023), wakati ambapo nyumbu hutawanyika kwenye maeneo ya miti na vichaka, hali inayowafanya kuwa vigumu kuonekana kwa njia ya picha za setilaiti.

“Ni vigumu sana kuona nyumbu kupitia picha za satellite wakiwa kwenye maeneo yenye miti mingi. Zaidi ya hapo, picha za setilaiti zinaathiriwa sana na mawingu na uoto wa asili,” alisema Dkt. Keyyu.

Tofauti ya Maeneo na Muda wa Picha

Aidha, TAWIRI hufanya sensa yake upande wa Tanzania pekee, katika eneo la takribani kilomita za mraba 4,782, wakati Duporge et al. walijumuisha maeneo ya Tanzania na Kenya kwa pamoja. Pia, TAWIRI hupiga picha nyakati za asubuhi wakati nyumbu wakiwa kwenye harakati za kutafuta chakula, tofauti na picha za satelaiti zinazopigwa mchana ambapo nyumbu huwa wamejificha kupumzika chini ya miti.

Hitimisho

TAWIRI imesema matokeo ya utafiti wa Duporge hayawezi kutumika wala kulinganishwa na sensa zake zilizotumia mbinu ya viwango vya kimataifa (Gold Standard), kwa sababu ya mapungufu mengi ya kiufundi yaliyojitokeza kwenye mbinu mpya ya satellite.

“Kwa njia waliyotumia, hawakuwa na uwezo wa kupata idadi halisi ya nyumbu. Hivyo, tunasisitiza kuwa takwimu hizo za 600,000 si sahihi na haziakisi uhalisia wa hali halisi,” alisema Dkt. Keyyu.

Amehitimisha kwa kusema kuwa wataalamu wa TAWIRI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kulifanyia kazi suala hilo na kutoa rai kwa umma kuwa na subira na kuzingatia taarifa sahihi kutoka kwa taasisi zinazotambulika kitaifa na kimataifa.

Chapisha Maoni

0 Maoni