Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha
Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema endapo wananchi wa Jimbo
hilo watamchagua tena kuwa mbunge wao atahakikisha anafanya jitihada ili wapate
maendeleo zaidi ikilinganishwa yale waliyoyapata katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita.
Dkt. Biteko amesema hayo
Septemba 11, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Katome
wilayani Bukombe mkoani Geita, ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa
Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“ Nataka niahidi, mkinichagua tena maendeleo tuliyoyapata
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tutazidisha mara mbili kwa miaka
mitano ijayo. Tunataka tuibadilishe
Bukombe na mnakumbuka tulikuwa na zahanati nne tu wilaya nzima, hatukuwa na
jengo la halmshauri na sasa tumejenga majengo yanayofanana na hadhi ya Wilaya
ya Bukombe,” amesema Dkt. Biteko.
Akitaja baadhi ya maendeleo iliyofikiwa wilayani humo
amesema ina zahanati zaidi ya 60, shule za sekondari za elimu ya upili tano
pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na Chuo Kikuu unaoedelea.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
Bukombe imebadilika kwa kiasi kikubwa na maendeleo yaliyofikiwa yatazidishwa
mara dufu katika miaka mitano ijayo na hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa
wingi kuwachagua wagombea wa CCM.
Kuhusu Kata ya Katome, Dkt. Biteko amesema Kata hiyo haikuwa
na mawasiliano ya simu, hospitali, umeme, barabara na shule ya sekondari
na iliwalazimu wanafunzi kwenda kusoma
Shule ya Sekondari ya Ushirombo.
Aidha, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia ilihakikisha
inajenga shule na kuwa na mpango wa kukarabati zilizokuwepo, inajenga zahanati
sambamba na kuipandisha hadhi zahanati iliyokuwepo kuwa kituo cha afya ili
kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.
Mipango ijayo ya CCM imetajwa kuwa ni pamoja na kujenga
barabara ya lami kuunganisha Kata ya
Katome na Mbogwe kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na hivyo kuwahakikishia
wananchi wakaopisha mradi huo malipo ya fedia
“ Mradi wa maji upo tayari tunataka tuupanue zaidi ili maeneo yote watu wapate maji na kazi hii
itafanyika mkituchagua, kuna vitongoji sita havina umeme, mkituchagua tena
tutaleta umeme kwenye maeneo hayo, tutaongeza minara ya mawasiliano nataka
niwaambie mkituchagua tena hamtatudai
hayo,”amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza
“Atakapokuja Rais Samia nataka tumwambie sisi tuko tayari kumpa kura
zote, ningependa kuona wapigakura wote 6,500 waliojiandikisha hapa Katome
kujitokeza kupiga kura, tunataka tulete maendeleo yanayoonekana si maneno.”
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Katome, Joseph Maganga amesema
kuwa CCM imetekeleza miradi mingi ikiwemo kujenga shule za sekondari na miradi
ya maji ili kutatua changamoto zilizokuwepo awali.
Hivyo amewahimiza wananchi wa Kata hiyo Oktoba 29 mwaka huu
kuwapigia kura wagombea wa CCM.



0 Maoni