Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi,
amemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Balozi Mohamoud Thabit Kombo, ameshiriki kwenye maadhimisho ya miaka 80 ya
Uhuru wa Vietnam yaliyofanyika jijini Dar Es Salaam. Maadhimisho hayo
yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuazimisha miaka 60 ya ushirikiano kati ya
Vietnam na Tanzania.
Mhe. Chumi
ameipongeza Vietnam kwa kuadhimisha
miaka 80 ya uhuru taifa hilo na miaka 60 ya ushirikiano mzuri uliopo wa
Kidiplomasia na Tanzania.
Mhe. Chumi
amesema maadhimisho hayo yanaakisi mafanikio makubwa yaliyopatikana kijamii na
kiuchumi kutokana na kufanya kazi kwa biddii, ustahilivu, na kufanya
mabadiliko. Kwa miaka 80 sasa Vietnam
imejenga uchumi thabiti, imara, na maendeleo endelevu. Vietnam inalenga
kufikia nchi iliyoendelea ifikapo mwaka 2045.
Tanzania na
Vietnam zinashirikiana katika maeneo ya uwekezaji, biashara, elimu, afya, kilimo pamoja na
maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa miongo sita iliyopita. Hivyo, Mhe. Chumi
emesema Tanzania inatambua na kuthamini juhudi, mchango wa kujitolea na
mapambano ya kihistoria baina ya Tanzania na Vietnam pamoja na wananchi wao.
Takwimu zinaonesha
kuwa Vietnam ni nchi ya saba kwa kuwa soko kubwa la bidhaa za Tanzania ambapo
mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda Vietnam yameongezeka kutoka Dola za
Kimarekani milioni 226.6 mwaka 2020 hadi Dola milioni 314.2 mwaka 2024 sawa na
ongezeko la asilimia 38 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kwa upande
wake, Balozi wa Vietnam nchini, Mhe. Vu Thanh Huyen ameeleza dhamira ya Vietnam
kuendeleza ushirikiano wa karibu na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kukuza
biashara, uwekezaji na maendeleo ya teknolojia kama njia ya kukuza uchumi wa
mataifa yote mawili.
Uhusiano wa
Kidiplomasia kati ya Tanzania na Vietnam ulianza tangu mwaka 1965, na
umefanikiwa kuimarisha ushirikiano wa uwili na wa kimataifa.
0 Maoni