Mgombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuimarisha sekta ya miundombinu nchini ikiwa
ni pamoja na barabara, reli na bandari kavu, ili kuongeza ufanisi wa
usafirishaji na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.
Akizungumza
leo Jumatano, Septemba 3, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la
Tunduma Mpakani, wilayani Momba mkoani Songwe, Mhe. Samia alisema kuwa Serikali
tayari imeanza kuchukua hatua za awali za kuboresha barabara na reli
zinazounganisha Tanzania na Zambia, ikiwa ni sehemu ya ajenda pana ya kuifanya
Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara ukanda wa Kusini mwa Afrika.
“Tumeanza
kazi ya maboresho ya miundombinu muhimu, na tunaendelea kuifanyia kazi reli ya
Tazara kwa ukarabati wa kiwango cha juu ili kuongeza kasi ya usafirishaji wa
mizigo. Tayari tumeshatia saini makubaliano na Serikali ya China kufanikisha
mradi huu muhimu,” alisema Samia mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza
kwenye mkutano huo.
Bandari kavu Mpemba kuondoa
msongamano
Katika hatua
nyingine, Samia alieleza kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa bandari kavu (dry
port) katika Kata ya Mpemba, Tunduma, yenye ukubwa wa ekari 1,800, ambayo
inalenga kupunguza msongamano wa malori na kurahisisha shughuli za usafirishaji
mipakani.
“Bandari hii
kavu itarahisisha biashara kati ya Tanzania na Zambia, pamoja na kupunguza muda
wa kusafirisha mizigo. Hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuifanya Tunduma kuwa
lango la kimkakati la kiuchumi,” alisema.
Samia pia
alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi wa mkoa wa Songwe na maeneo ya mpakani
kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi kwa amani, huku akisisitiza kuwa
Serikali ya CCM itaendelea kujenga miundombinu bora inayogusa maisha ya
wananchi wa kawaida.
0 Maoni