Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 13, 2025 amezindua kampeni za Ubunge
jimbo la Nachingwea zilizofanyika katika uwanja wa maegesho ya Malori
Nachingwea mjini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Majaliwa
ametoa wito kwa wananchi kuchagua wagombea wote wa chama cha mapinduzi ifikapo
Oktoba 29 mwaka huu ili waendee kuitekeleza ilani uchaguzi ya CCM ya mwaka
2025/2030 na kuiwezesha Nachingwea kuendelea kupaa kwa kasi kimaendeleo.
“Jitokezeni kwa wingi kwenda kupiga kura ifikapo oktoba 29,
nendeni mkamchague Rais Dkt. Samia kwa kura nyingi, kamchagueni pia Fadhili
Liwaka hatupaswi kulala, hata kama ni mgombea pekee nendeni mkaweke tiki muda
utakapofika.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Wilaya za Ruangwa na
Nachingwea zimeendelea kunufaika na miradi ya maendeleo ikiwemo mradi mkubwa wa
maji kutoka Nyangao, Ruangwa hadi Nachingwea ambao unaendelea kutekelezwa.
“Mradi huu utakaonufaisha vijiji vya Ruangwa ma Nachingwea utagharimu shilingi
bilioni 119.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa tayari Serikali
imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Ruangwa hadi
Nachingwea.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa amefanya kazi kwa karibu na Liwaka kwa kipindi kirefu, na anamfahamu kwa uchapakazi wake na anaamini atajitoa kwa ajili ya maendeleo ya wananachingwea. Ninamfahamu Liwaka, anajua namna ya kuchapa kazi.”
Kwa upande wake, mgombea ubunge jimbo la Nachingwea Fadhili
Liwaka amesema kuwa katika kipindi chake atajielekeza katika sekta za
kimaendeleo ikiwemo Miundombinu, Elimu, Afya, Kilimo na Ufugaji.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu moja ya kiu yangu kubwa katika sekta
ya miundombinu ni ujenzi wa barabara ya Nachingwea hadi Masasi kwa kiwango cha
lami, pamoja na hili, elimu ni agenda kubwa niliyonayo ninataka kupunguza idadi
ya wanafunzi hasa wa kike wanaolala nyumbani na kwenda shuleni asubuhi kwa
kujenga mabweni”.
Pia, Liwaka amesema kuwa moja ya ndoto yake kubwa aliyonayo ni kuhakikisha anamaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji. “Mheshimiwa Waziri Mkuu ninatamani siku moja tufanye sherehe wafugaji walete ng’ombe tuchinje na wakulima walete mahindi tupike tusherehekee”.



0 Maoni