Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka wataalam wa ufuatiliaji na tathmini nchini kufanya kazi yao kwa
kizingatia misingi ya kitaaluma ili kuleta matokeo.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 12, 2025 wakati
akimwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah
kufunga Kongamano la nne la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) lililofanyika
Jijini Mwanza.
“ Mnapofanya kazi zenu msijione wanyonge wala msitafute
kupendwa bali tendeni haki kwa kutuonesha udhaifu uliopo na kuonesha ukweli ili
- ufanyiwe kazi,” amesema Dkt. Biteko.
Amewahimiza wataalam hao kufanya kazi bila kuhurumiana na
badala yake kuwa wakweli kwa kuonesha mafanikio nanudhaifu uliopo ili kuleta
ufanisi.
Katika hatua nyingine, amewapongeza wataalam wa ufuatiliaji
na tathmini kwa kutekeleza maazimio ya mwaka uliopita kwa asilimia 78 na
kuongeza kwa kuwataka kuongeza nguvu zaidi katika sekta hiyo.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri ya thathmini ya maazimio
yaliyofikiwa mwaka jana, lakini tunahitaji zaidi kutoka kwenu.” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Doto Biteko amewaelekeza waajiri, wakurugenzi na
wakuu wa idara na vitengo kuwapeleka wataalam wao katika mafunzo zaidi ya
kitaalam ili waweze kupata mbinu na ujuzi wa kufanya majukumu yao kwa ufanisi
zaidi.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge
na Uratibu, Dkt. James Kilabuka amesema Kongamano la mwaka huu limewavutia
washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
“Mwaka huu tumepata washiriki zaidi ya 1,200 ikilinganishwa
na washiriki 954 wa mwaka jana,” amesema Dkt. Kilabuka.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuimarisha uwezo wa Ufuatiliaji
na Tathmini kwa Jamii ili kuwezesha utendaji bora na Maendeleo endelevu”.



0 Maoni