Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya
Madini imekutana na wataalam kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Kitengo cha
Kudhibiti Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit – FIU) kwa lengo la
kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti utakatishaji
fedha katika sekta ya madini.
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Tume ya Madini
jijini Dodoma kimekusudia kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo tatu ili
kuzuia mzunguko wa fedha haramu kupitia miamala ya wadau wa sekta ya madini.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi
na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, Annasia Kwayu, amesema kuwa
ushirikiano huo utasaidia kuongeza uwazi na ufanisi katika mnyororo mzima wa
biashara ya madini.
Ameongeza kuwa Tume inatambua na kuthamini mchango wa FIU
katika kutoa miongozo na mafunzo yanayosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya
utakatishaji wa fedha haramu.
“Tumejadili masuala mbalimbali na wenzetu kutoka BOT na FIU.
Jambo kubwa ni kudhibiti utakatishaji fedha katika sekta ya madini ili kulinda
heshima ya nchi kimataifa na kuongeza mchango wa sekta hii katika kukuza uchumi
wa nchi,” amesema Kwayu.
Kwa upande wake, Dkt. Anna Lyimo kutoka Benki Kuu (BoT)
amesema Benki Kuu, kama ilivyo kwa benki kuu za mataifa mengine, ina jukumu la
kusimamia sera ya fedha na kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.
“BoT imejipanga kikamilifu kudhibiti mianya ya utakatishaji
wa fedha haramu katika zoezi la ununuzi wa asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa
nchini, na tupo tayari kushirikiana na Tume ya Madini ili kuhakikisha nchi
inaendelea kuaminika kimataifa na kukuza uchumi wake,” amesema Dkt. Lyimo.
Naye Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU),
Majaba Magana, amesisitiza kuwa Tume ya
Madini kama taasisi yenye dhamana ya kudhibiti utakatishaji fedha katika sekta
ya madini, inatakiwa kuimarisha mifumo yake ikiwemo kuandaa miongozo ya
utekelezaji ikiwa ni sehemu ya Mwongozo wa Usimamizi uliotolewa na FIU.
“Kwa upande wetu, tupo tayari kutoa ushirikiano wa karibu, ikiwemo kusaidia katika utoaji wa elimu kwa wadau wa sekta ya madini ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo,” amesema Magana.




0 Maoni