Mahakama Kuu Masijala Kuu-Dodoma, imemrejesha kwenye mbio za
kuwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mgombea urais wa
chama cha ACT-Wazalendo Luhaga Mpina.
Katika hukumu yao, majaji wamesema Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi (INEC) ni huru na haikupaswa kusikiliza maelekezo ya mtu au taasisi
yoyote, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Katika kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na jopo la majaji
watatu, Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza, Mahakama Kuu pia
wamesema kwa kutopokea fomu za Mpina, Tume ilimnyima haki ya kikatiba na ile ya
kusikilizwa.
Vile vile Majakama Kuu imebatilisha barua ya Tume ya kumzuia
Mpina kurejesha fomu kwa kuwa ilikuwa kinyume cha Katiba na haikuwa na nguvu ya
kisheria.
Mahakama imeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) impe
nafasi mgombea huyo wa ACT-Wazalendo kuwasilisha
fomu zake na mchakato uendelee ulipoishia Agosti 27, 2025.
Mpina alikuwa anapinga kuenguliwa katika mbio za urais
kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025 ambapo INEC ilimzuia kuingia kwenye ofisi za tume
kukabidhi fomu zake na kuteuliwa.
INEC ilichukua uamuzi huo, kutokana na taarifa ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kuwa mgombea huyo hakukidhi vigezo vya kuteuliwa ndani ya ACT-Wazalendo, baada ya kupingwa na kada wa chama hicho.

0 Maoni