WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa shughuli za
ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu ya kuliwezesha Taifa kufanikisha na
kufikia malengo mbalimbali ya kimaendeleo.
Amesema kuwa ni ukweli usiopingika wadau wote na jamii
kwa ujumla wakiwa na uelewa wa pamoja kuhusu shughuli za ufuatiliaji na
tathmini matokeo ya haraka yatapatikana.
Amesema hayo leo Alhamisi (Septemba 11, 2025)
alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kongamano la
Nne la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza linalofanyika katika
ukumbi wa hotel ya Malaika Beach jijini Mwanza.
Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za
kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ikiwa ni kutekeleza kwa vitendo
maono ya Rais Dkt. Samia ya kuimarisha upimaji wa utendaji wa Taasisi za Umma,
uwajibikaji na kuongeza kasi na uwazi katika kutoa huduma na ustawi wa wananchi
kwa ujumla.
“Shughuli za ufuatiliaji na tathmini zinahusisha ukusanyaji,
uchambuzi na upimaji wa taarifa kuhusu shughuli zilizopangwa, utekelezaji na
matokeo yaliyopatikana. Serikali imekuwa na utaratibu wa kufanya shughuli hii
katika vipindi mbalimbali.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Idara
zote zenye dhamana zihakikishe zinakamilisha maandalizi ya Sera ya Taifa ya
Ufuatiliaji na Tathmini kwa upande wa Serikali zote mbili ili kuwezesha
kutungwa kwa Sheria inayokwenda kuongoza Ufuatiliaji na Tathmini
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Ofisi ya Waziri Mkuu
pamoja na Mamlaka ya Serikali Mtandao kukamilisha Maandalizi ya Mfumo Jumuishi
wa Ufuatiliaji na Tathmini wa kielektroniki. Utakuwa Mfumo Mkuu wa Mifumo yote
ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji ndani ya Serikali lengo ni
kuweza kuzifuatilia idara za Serikali vizuri, na utawezesha viongozi, watoa
maamuzi na wananchi kupata taarifa na takwimu sahihi na kwa muda.
“Watendaji wakuu wote tumieni taarifa zinazozalishwa
kutokana na kazi za ufuatiliaji na tathmini ili mfanye maamuzi
na kuweka mikakati imara ya kuhabarisha umma juu ya matokeo ya
utekelezaji wa kazi za Serikali kwa uhakika zaidi.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa
Chama cha Wataalamu wa Tathmini Afrika (AfrEA), kuendelea kuzilea TanEA
(Tanzania) na ZaMEA (Zanzibar) kwa kuzipa uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu
yao ikiwemo kuwaongoza katika mabadiliko ya kiteknolojia ya utunzaji takwimu na
ufuatiliaji.
“TanEA na ZaMEA, endeleeni kujiimarisha na kuongeza kasi ya
kuwaunganisha wadau wote muhimu kwa lengo la kubadilishana mawazona uzoefu au
kujadili mbinu mpya na bora za zitakazowawezesha kuwafikisha kufanikiwa katika
kufanya ufuatiliaji na tathmini wake”.
kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,
Bunge na Uratibu William Lukuvi amesema kuwa katika jitihada zakuimarisha
Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini nchini,Ofisi ya Waziri Mku kwa kushirikiana
na Mamlaka Mtandao – eGA imefanikiwa kuanza ujenzi wa mfumo wa Kitaifa wa
Kielektroniki waufuatiliaji na tathmini “Government Wide Electronic Monitoring
and Evaluation System”ambao utapokea taarifa kutoka mifumo mingine na
kuzichakata na kuwezesha maandalizi yataarifa ya utendaji wa Serikali.
“Uwepo wa Mfumo huo utawezesha kupokea data, kuzichakata, kuzitafsiri
kwa wakati na kuiwezesha Serikali katika ngazi zote kutumia takwimu sahihi
katikakupanga, kuboresha afua zinazotekelezwa nakuamua kwa usahihi”.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu
Dkt. Jim Yonaz amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliweka
msingi imara wa kuimarisha shughuli za ufuatiliaji na tathmini kwa kuanzisha
Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali.
Amesema kiwa Idara hiyo imeendelea kuwa idara nguzo na
muhimu katika kuchangia na kuendeleza juhudi za kuboresha utaalamu wa kufanyia
tathmini nchini ambayo imewezesha mashirika ya umma na taasisi mbalimbali
kujifunza kutoka katika idara yetu hiyo. “Na tunaamimi kwamba si tu ndani ya
nchi bali imeendelea kuwa mwanga hata nje ya nchi, hii ndio nia yetu ya
kuifanya iwe kituo cha kujifunza na maarifa.”
Kwa Upande wake Muwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Suzan Ngongi amesema kuwa uwazi na uwajibikaji umeiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta za elimu, afya, miundombinu pamoja na mipango ya kupambana na umasikini “Jitihada hizi zimeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.”



0 Maoni