Tume ya
Madini imeendelea kutoa elimu kwa wachimbaji kuhusu matumizi ya Kigida
(Retort), kifaa kinachosaidia kulinda afya za wachimbaji, mazingira na
kupunguza gharama za matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu.
Akizungumza
kwenye Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika
Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, Afisa Mazingira
Mwandamizi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Hyasinta
Rugeiyamu, amesema Kigida kimeundwa kwa mfumo unaozuia mvuke wa zebaki kuingia
mwilini wakati wa uchenjuaji, hivyo kumlinda mchenjuaji dhidi ya madhara ya
kiafya.
“Mbali na
kulinda afya, Kigida huzuia pia moshi wa zebaki kutawanyika hewani. Badala
yake, mvuke huo hubadilishwa kuwa kimiminika kinachohifadhiwa na kutumika tena.
Hii husaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na gharama za ununuzi wa zebaki
mpya,” amefafanua Rugeiyamu.
Ameongeza
kuwa Tume ya Madini itaendelea kuhamasisha wachimbaji kote nchini kutumia
Kigida ili kuhakikisha shughuli za uchenjuaji zinafanyika kwa usalama,
tija na uendelevu.




0 Maoni