INEC yawarejesha wagombea 22 katika mbio za uchaguzi

 

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetengua baadhi ya maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi kuhusu uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani kwa uchaguzi wa mwaka huu, na kuwarejesha wagombea 22 katika orodha ya wagombea watakaoshiriki uchaguzi mkuu. 

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima Ramadhani Kailima, amesema kuwa tume ilipokea jumla ya rufaa 51 za kupinga uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi kuhusu pingamizi za uteuzi wa wagombea, ambapo 20 zilihusu ubunge na 31 zilihusu nafasi za udiwani. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rufaa hizo zilipokewa kwa mujibu wa Kifungu cha 53 na 65 vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, pamoja na Kanuni ya 29(1) ya Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2025. 

Tume Yarejesha Wagombea Wanne wa Ubunge 

Katika kikao chake kilichofanyika kuanzia Septemba 1 hadi 3, 2025, Tume ilikubali rufaa nne za ubunge, ambapo wagombea waliorejeshwa katika kinyang’anyiro ni: 

Mvungi Lucas Felix – NCCR-Mageuzi, Jimbo la Mwanga

Anaeli Roiya Nasari – ACT-Wazalendo, Arumeru Mashariki

Ngwada Mubarak Twaha – CHAUMMA, Mafinga Mjini

Matiko Esther Nicholas – CCM, Tarime Mjini 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Tume imetengua maamuzi ya awali ya wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo hayo na wagombea hao sasa wanaruhusiwa rasmi kuendelea na kampeni za uchaguzi. 

Aidha, kwa Jimbo la Tarime Mjini, Tume imeamua kumuondoa Kangoye Jackson Ryoba wa ACT-Wazalendo katika orodha ya wagombea, na kumtambua Matiko Esther Nicholas wa CCM kuwa mgombea halali. 

Rufaa Saba za Ubunge Zakwama 

Tume pia imekataa rufaa saba za ubunge, ambapo wagombea waliokataliwa ni: 

Gimbi Dotto Masaba (CHAUMMA – Itilima)

Omary Ahmad Badwel (CHAUMMA – Bahi)

Mohamed Juma Haji (AAFP – Chambani)

Loyce Benjamin Giboma (CHAUMMA – Ubungo)

Pius Ismail Masuruli (ACT-Wazalendo – Bunda Mjini)

Kangoye Jackson Ryoba (ACT-Wazalendo – Tarime Mjini)

Salum Khamis Salum (CCM – Meatu)

Tume imeeleza kuwa imeafiki uamuzi wa awali wa wasimamizi wa uchaguzi kutowateua wagombea hao kutokana na sababu mbalimbali za kisheria. 

Mgombea Ajitoa, Rufaa Yafutwa 

Katika hatua nyingine, rufaa ya Flatei Gregory Massay (ACT-Wazalendo – Mbulu Vijijini) ilifutwa na Tume baada ya mgombea huyo kujiondoa rasmi katika kinyang’anyiro, hali iliyosababisha rufaa yake kupitwa na wakati kwa mujibu wa sheria. 

Wagombea 9 wa Udiwani Wapewa Neno la Kuendelea 

Katika upande wa udiwani, Tume imekubali rufaa tisa (9), na kuwarejesha wagombea waliokuwa wamewekewa pingamizi. Miongoni mwa waliorejeshwa ni: 

Abdurahamani Matulano – ACT-Wazalendo (Mijelejele, Lulindi)

Anafi Salumu Nandala – ACT-Wazalendo (Ndomoni, Nachingwea)

Lulu Omari Bakari – NCCR-Mageuzi (Rahaleo, Lindi Mjini)

William Baliyakula – ACT-Wazalendo (Buseresere, Chato Kusini)

Mackrina Chales Nyoni – ACT-Wazalendo (Mkongo, Namtumbo)

na wengine... 

Tume imeeleza kuwa wagombea hao sasa wako huru kuendelea na kampeni kwenye kata zao.

 Rufaa 17 za Udiwani Zakataliwa 

Wakati huo huo, wagombea 17 wa udiwani walikataliwa na Tume baada ya kushindwa katika rufaa walizowasilisha. Hawa ni pamoja na: 

Rafii Kibwana Kombo (CHAUMMA – Pangani Mashariki) 

Abasi Kambi Legeza (ACT-Wazalendo – Visiga)

Sophia Ally Magimba (ACT-Wazalendo – Mzenga)

Moses Marwa Mwera (ACT-Wazalendo – Muriba)

Zephania Godeni Chibaya (CHAUMMA – Songambele) 

na wengineo...

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume, maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi wa kata hizo yameungwa mkono kwa misingi ya sheria na kanuni. 

Waliothibitishwa waendelee na Kampeni 

Tume pia imewatangaza baadhi ya wagombea kuwa waliopitishwa rasmi na kwamba pingamizi dhidi yao hazina mashiko. Miongoni mwao ni: 

Esther Ernest Bulaya (CCM – Bunda Mjini)

Rosemary Kasimbi Kirigini (ACT-Wazalendo – Meatu)

Job Isaack Ibrahim (CCM – Mzinga)

 na wengineo katika kata mbalimbali.

 Wagombea hao sasa wataendelea na kampeni zao za kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 25 Oktoba 29 2025.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni