Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewanasihi Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi kuendelea kushikamana, kuishi kwa umoja na kusaidiana ili kupata baraka za Mwenyezi Mungu.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo aliposhiriki Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qurani, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Taasisi ya Altijarah Al Arabiha ya Oman na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, yaliyofanyika katika Msikiti wa Jamiu Zanzibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kujipamba na Qurani, kuishi kwa maadili mema, kusaidiana, kupendana, kuzingatia malezi bora ya vijana pamoja na kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameipongeza Taasisi ya Altijarah Al Arabiha ya Oman na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa mafanikio ya mashindano hayo na mchango wao katika kusaidia jamii kupitia elimu, afya, chakula na huduma za kiafya, huku akihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mashindano hayo yameshirikisha washiriki sita kutoka Ujerumani, Uganda, Tanzania, Urusi, Canada na Brazil, ambapo Nd. Usama Barghouth kutoka Ujerumani ameibuka mshindi wa kwanza na kutunukiwa kombe, cheti na zawadi ya shilingi milioni 20.


.jpeg)
0 Maoni