Serikali
imeongeza ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja
na shughuli zote za mnyororo mzima wa thamani wa madini nchini ambapo kwa Mkoa
wa Geita pekee wachimbaji wadogo wamezalisha kilo 22,014.61 zenye thamani ya
shilingi trilioni 3.443 na Serikali kukusanya mapato ya shilingi bilioni 2.5
katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025.
Mchango
wa wachimbaji wadogo wa madini umeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2020 hadi
kufikia asilimia 40 mwaka 2024 katika mapato yote ya sekta ya madini na mchango
wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka
2020 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2024.
Akizungumza
jana Septemba 28, 2025 katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili
mkoani Geita wakati akifunga Maonesho ya Nane ya Teknolojia na Uwekezaji katika
Sekta ya Madini, yenye kauli mbiu “Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya
Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora/Shiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba
2025”. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amewapongeza wachimbaji wadogo na Wizara ya Madini kwa hatua hiyo.
“ Napenda
kutoa pongezi maalum kwa Wizara ya Madini kwa usimamizi mzuri wa sekta hii
pamoja na wachimbaji wadogo wa Tanzania. Ninyi ni sababu ya kusheherekea
mafanikio haya mmekuwa shamba darasa na baada ya Serikali kuwapatia nafasi
mmeonesha kwa vitu mlivyofanya mkipewa fursa mnaweza,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea
“Mmepambana sana kuleta teknolojia ndani ya nchi na mmeonesha Watanzania
wanaweza kufanya mambo makubwa na wakafanikiwa.”
Aidha,
amesema kuwa tangu kuanza kwa maonesho hayo mwaka 2018 kumekuwepo na mabadiliko
makubwa ya kiteknolojia yanayochangia kuongezeka kwa kasi ya uzalishaji madini
hasa kwa wachimbaji madini wadogo. Ambapo katika uchenjuaji madini, zimekuwepo
teknolojia mbalimbali za kisasa zikiwemo Carbon – In – Leach (CIL), Carbon - In
– Pulp (CIP) na Froth Floatation (FF) ambazo zimekuwa na tija zaidi kuliko
matumizi ya zebaki ambayo imekuwa na athari nyingi za kiafya na mazingira
sambamba na kiwango kidogo cha uzalishaji.
Dkt.
Biteko amesema kufuatia usimamizi thabiti na mabadiliko makubwa ya teknolojia
ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uwepo wa maonesho hayo ya teknolojia,
Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi
trilioni 3.8 kwa kipindi cha miaka minne
kuanzia mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025.
Akizungumzia
hatua mbalimballi za Serikali katika kuhamasisha uongezaji thamani madini, Dkt.
Biteko amesema kumekuwepo na uanzishwaji wa viwanda vya uyeyushaji na
usafishaji wa madini ya dhahabu, nikeli na shaba katika maeneo mbalimbali
nchini ambapo kwa sasa kuna jumla ya viwanda nane vya uchenjuaji wa shaba na
nickel katika Mkoa wa Dodoma, Kiwanda kimoja cha Uyeyushaji wa Shaba (Chunya)
na Viwanda Sita vya Usafishaji wa Dhahabu katika Mikoa ya Geita, Mwanza na
Shinyanga-Kahama.
“ Nitoe
wito kwa wachimbaji na Wizara kuendelea kubuni na kuongeza uwezeshwaji wa
Watanzania kuongeza thamani ya madini wanayozalisha. Mazingira haya yataongeza
upatikanaji wa fedha za kigeni pamoja na kuwapatia watanzania ajira kwenye
viwanda vya uongezaji thamani, STAMICO mmefanya kazi kubwa sana kubadilisha na
kushiriki kwenye local content.” amesisitiza Dkt. Biteko.
Amewahakikishia
kuwa Serikali sikivu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya
maendeleo ya sekta ya madini ikiwemo kufikisha huduma ya umeme katika maeneo
yote muhimu.
Fauka ya
hayo, Dkt. Biteko amewaasa washiriki wa maonesho hayo kushiriki kikamilifu
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuwa hatua hiyo ni muhimu katika nchi
ya kidemokrasia.
Naye,
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ambapo mwaka jana aliagiza uwanja huo wa
maonesho ujengewe miundombinu ya kudumu.
Amesema
agizo hilo limetekelezwa na sasa uwanja huo una mabanda tisa ya kudumu ikiwa ni
awamu ya kwanza ya ujenzi.
Amesema
maonesho hayo kwa mwaka huu yamehudhuriwa na washiriki 930
wakiwemo washiriki kutoka nje ya
nchi ikilinganishwa na washiriki 600 mwaka 2024.
Amesema
“Rais Samia amewezesha kutoa leseni 9,000 kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wa
Pori la Kigosi na sasa tumeweza kuzalisha zaidi ya tani 22,000 za madini kwa
wachimbaji wadogo.”
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi
Zena Said amewashauri wadau wa sekta ya madini kwa ujumla kutumia fursa za
taasisi za fedha ili kupata elimu kuhusu masuala ya fedha na uwekezaji.
Akimwakilisha
Waziri wa Madini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema
maonesho hayo yamekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kuwa chachu hususan kwa
wachimbaji wadogo na kuwaongezea elimu kuhusu uchimbaji hatarishi na matumizi
ya zebaki.
Vilevile
amesema Wizara ya Madini itahakikisha inasimamia sheria na taratibu zote ili
kufanya sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo amesema kuwa hivi sasa sekta ya madini
nchini imefikia kiwango cha kushawishi viwanda vya kuzalisha vipuri kuja
kuwekeza Tanzania ili vipuri hivyo vipatikane nchini na kufikia lengo la kuwa
na Tanzania ya viwanda.
Amebainisha
kuwa Tume ya Madini itaendelea kuwezesha sekta ya madini ili kuhakikisha madini
yanawanufaisha Watanzania wote.
Mwenyekiti
wa Wachimbaji Wadogo, Lenard Bugomola
amesema kuwa Mkoa wa Geita umekuwa ukiongoza kwa uzalishaji wa dhahabu,
aidha ameomba STAMICO iwapatie mitambo miwili ya uchimbaji madini.
Awali
Dkt. Biteko alitembelea mabanda ya mbalimbali yakiwemo Taasisi ya Jiolojia na
Utafiti wa Madini, Anglo Gold Ashanti, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO),
Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Mwamba Mining ambapo
alielezwa kuhusu teknolojia ya kisasa ya uchimbaji madini.
Na. Ofisi
ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni