Katibu
Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amekabidhi mabomu
baridi mia nne (400), pikipiki mbili na ndegenyuki (drone) moja kwa kituo cha
askari uhifadhi Goha wilayani Korogwe mkoani Tanga kwa ajili ya kukabiliana na
changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.
Akikabidhi
vifaa hivyo jana Septemba 28, 2025 Dkt. Abbasi amesema hiyo ni hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa
Mkakati wa Kitaifa wa kudhibiti mwingiliano wa binadamu na wanyamapori ili
kupunguza madhara kwa jamii.
“Mnafahamu
nchi nzima kuna maeneo mengi yenye changamoto za muingiliano wa wanyama wakali
na waharibifu ambao wanaharibu mazao,
mimea mingine na wanashambulia binadamu
hivyo kama Wizara tuna mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na changamoto
hiyo” amesisitiza Dkt. Abbasi.
Amesema
Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo
kisayansi na kioparesheni ikiwa ni pamoja na kuchimba mabwawa ikiwepo ya Wilaya ya Same, kutumia helikopta
kuwarudisha wanyama hifadhini na kutumia ndegenyuki ambazo zilishakabidhiwa
katika kituo hicho na kote nchini.
“Tunaamini
vifaa hivi vitaongeza ufanisi wa kuwafukuza hasa wanyama wakali kama tembo ili
wananchi wetu wazidi kuwa salama na waweze kufanya shughuli zao kwa amani”
amefafanua Dkt. Abbasi.
Dkt.
Abbasi amewaomba Wananchi kuzingatia maelekezo wanayopewa wakati wa kukabiliana
na changamoto hiyo na pia kutoa taarifa kwa askari kupitia namba maalum za
askari inayotumika katika wilaya zote ili kuepusha taharuki.
Naye,
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Bw.
Emmanuel Moirana ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kukabidhi vifaa
hivyo na kusisitiza kuwa vitaenda kutatua changamoto ya Wanyama wakali na
waharibifu kwa kuwa ni kubwa katika eneo hilo.
Ameongeza
kuwa lengo ni kuboresha ufukuzaji wa tembo, kuongeza upataji wa taarifa sahihi
tembo walipo na kubaini chanzo cha tatizo hivyo amewaomba wananchi kutoa
ushirikiano wa kutosha ili kupunguza madhara ya tembo.
Makabidhiano
hayo ni muendelezo wa utekelezaji wa mkakati wa kukabiliana na wanyamapori
wakali na waharibifu nchini.
Na
Mwandishi Wetu- Goha Korogwe



0 Maoni