Shinikizo la damu lisilodhibitiwa lawaweka watu zaidi ya bilioni moja katika hatari

 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa ripoti yake ya pili ya kimataifa kuhusu shinikizo la damu (Global Hypertension Report), ikiainisha kuwa watu bilioni 1.4 waliishi na shinikizo la damu mwaka 2024, huku ni zaidi ya mmoja tu kati ya watano aliyefanikiwa kuidhibiti hali hiyo kwa dawa au kubadili mienendo ya afya.

Ripoti hiyo mpya, iliyozinduliwa katika mkutano maalumu ulioandaliwa kwa ushirikiano wa WHO, Bloomberg Philanthropies na taasisi ya Resolve to Save Lives pembeni mwa Mkutano Mkuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa, imeonesha pia kuwa ni asilimia 28 tu ya nchi zenye kipato cha chini ndizo zimeripoti kuwa dawa zote zinazopendekezwa na WHO dhidi ya shinikizo la damu zinapatikana kwa ujumla katika maduka ya dawa au vituo vya afya vya msingi.

“Kila saa, zaidi ya watu 1,000 hufariki kwa sababu ya kiharusi na mshtuko wa moyo unaotokana na shinikizo la damu la juu – na vifo vingi vinaweza kuzuilika,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. “Nchi zina zana za kubadili simulizi hili. Kwa dhamira ya kisiasa, uwekezaji endelevu na mageuzi katika huduma za afya, tunaweza kuokoa mamilioni ya maisha na kuhakikisha huduma za afya kwa wote.”

Gharama ya Kimataifa kwa Uchumi na Maisha

WHO imeonya kuwa bila hatua za haraka, mamilioni ya watu wataendelea kufariki mapema na nchi zitakabiliwa na hasara kubwa za kiuchumi. Kati ya mwaka 2011 hadi 2025, magonjwa ya moyo na mishipa (ikiwemo shinikizo la damu) yanakadiriwa kugharimu nchi za kipato cha chini na cha kati kiasi cha Dola za Kimarekani trilioni 3.7 — sawa na asilimia 2 ya jumla ya pato lao la taifa.

Shinikizo la damu linaendelea kuwa chanzo kikuu cha mshtuko wa moyo, kiharusi, maradhi ya figo ya muda mrefu na ugonjwa wa kusahau (dementia). Ugonjwa huu unaweza kuzuilika na unatibika, lakini vikwazo vingi vinazuia hatua madhubuti.

“Shinikizo la juu la damu lisilodhibitiwa husababisha zaidi ya vifo milioni 10 kila mwaka, licha ya ukweli kuwa linaweza kuzuilika na kutibiwa,” alisema Dkt. Kelly Henning, kiongozi wa Programu ya Afya ya Umma ya Bloomberg Philanthropies. “Nchi zinazojumuisha matibabu ya shinikizo la damu katika huduma za afya kwa wote na ngazi ya msingi zinaendelea vizuri, lakini bado mataifa mengi ya kipato cha chini na kati yameachwa nyuma.”

Vikwazo Vinavyokwamisha Mafanikio

Takwimu kutoka nchi 195 na maeneo mbalimbali duniani zinaonesha kuwa nchi 99 zina viwango vya udhibiti wa shinikizo la damu chini ya asilimia 20. Idadi kubwa ya walioathirika wanaishi katika nchi za kipato cha chini na kati, ambako mifumo ya afya imelemewa na ukosefu wa rasilimali.

Ripoti hiyo imebainisha pengo kubwa katika uzuiaji, utambuzi, matibabu na huduma za muda mrefu kwa wagonjwa wa shinikizo la damu. Miongoni mwa changamoto kuu ni:

·         sera dhaifu za kuhamasisha afya kuhusu hatari kama vile unywaji wa pombe, matumizi ya tumbaku, kutofanya mazoezi, ulaji wa chumvi na mafuta mabaya;

·         upatikanaji mdogo wa vifaa sahihi vya kupima shinikizo la damu;

·         ukosefu wa miongozo ya matibabu na timu za huduma ya msingi zilizopewa mafunzo;

·         upungufu wa dawa na gharama kubwa;

·         ukosefu wa mifumo madhubuti ya taarifa kufuatilia mwenendo wa ugonjwa.

Dawa: Silaha Muhimu Katika Mapambano

Dawa za kudhibiti shinikizo la damu zinatajwa kuwa kati ya zana bora zaidi na za gharama nafuu katika afya ya umma. Lakini kwa nchi zenye kipato cha chini, ni 7 tu kati ya 25 (asilimia 28) ndizo zimeripoti kupatikana kwa dawa zote zinazopendekezwa na WHO — ikilinganishwa na asilimia 93 kwa nchi tajiri.

“Dawa salama, bora na za bei nafuu za kudhibiti shinikizo la damu zipo — lakini watu wengi hawawezi kuzipata,” alisema Dkt. Tom Frieden, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Resolve to Save Lives. “Kufunga pengo hilo kutasaidia kuokoa maisha — na pia kuokoa mabilioni ya dola kila mwaka.”

Mafanikio ya Nchi Zinazoongoza

Pamoja na changamoto nyingi, ripoti imeonesha kuwa maendeleo yanawezekana. Nchi kama Bangladesh, Ufilipino na Korea Kusini zimepiga hatua kubwa kwa kuingiza huduma za shinikizo la damu kwenye huduma za afya kwa wote, kuwekeza katika afya ya msingi na kushirikisha jamii:

·         Bangladesh: Imepandisha viwango vya udhibiti wa shinikizo kutoka asilimia 15 hadi 56 kati ya mwaka 2019 na 2025 katika baadhi ya maeneo, kwa kujumuisha huduma hizi katika huduma muhimu za afya.

·         Ufilipino: Imetekeleza kwa mafanikio kifurushi cha kiufundi cha WHO cha HEARTS katika huduma za ngazi ya jamii nchini kote.

·         Korea Kusini: Mageuzi ya afya yamechangia upatikanaji wa dawa kwa bei nafuu, kupunguza ada kwa wagonjwa, na kuongeza udhibiti wa shinikizo hadi kufikia asilimia 59 mwaka 2022.

Wito kwa Nchi Zote

WHO imezitaka nchi zote kujumuisha udhibiti wa shinikizo la damu katika mageuzi ya huduma ya afya kwa wote (UHC), ikiainisha kuwa utekelezaji wa hatua zilizopendekezwa unaweza kuzuia vifo vya mapema kwa mamilioni na kupunguza gharama kubwa za kijamii na kiuchumi kutokana na tatizo hilo.

Chapisha Maoni

0 Maoni