Mgombea
Ubunge wa Jimbo la Bukombe kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto
Mashaka Biteko amesema kuwa kwa Serikali ya CCM inayoongozwa na Dkt. Samia
Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya
ya Bukombe ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za kukuza uchumi wa Wilaya hiyo.
Dkt.
Biteko amesema hayo Septemba 27, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata
ya Katente wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema
mwaka 2015 Kata ya Katente, Igulwa na Kata zote zilizopo maeneo ya mjini
zilikuwa na kiwango duni sana cha maendeleo ikilinganishwa na maendeleo
yaliyofikiwa sasa.
Amesema Wilaya ya Bukombe ilikuwa na shule
moja ya kidato cha tano na sita, hospitali moja, zahanati nne huku umeme ukiwa
katika vijiji saba pekee.
Amesema
Serikali ya CCM imekuwa ikifanya jitihada kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuboresha
maisha ya wananchi wa Wilaya hiyo ambapo sasa inajenga jengo la Ofisi ya Mkuu
Wilaya, jengo la halmashauri, soko na stendi ya kisasa.
“ Rais
samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo kwenda Katoro
kwa kiwango cha lami ambao unaendelea na
ameruhusu watu kuchimba dhahabu katika Pori la Kigosi na sasa vijiji vyote
vimepelekewa umeme,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza
kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali “ Tunajenga Chuo
cha VETA pamoja na Chuo Kikuu vyote hivi vitasaidia kuleta mzunguko wa fedha na
kukuza uchumi wetu, watu hawataki maneno wanataka maendeleo na Dkt. Samia
amedhamiria kuibadilisha Bukombe.”
Sambamba
na hayo, Dkt. Biteko amewahimiza wananchi wa Katente 19,000 waliojiandikisha
kupiga kura ifikapo Oktoba 29 wamchague Dkt. Samia kwa nafasi ya Urais, mbunge
na diwani wa CCM ili kuendelea kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Bukombe.
Akizungumzia
katika mkutano wake wa kampeni Kata ya Bulangwa, Dkt. Biteko amesema kuwa Dkt.
Samia amesaidia sana kuleta maendeleo katika Kata hiyo na kuwa miaka mitano
iliyopita alitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
“ Hapa
Bulangwa tumejenga shule ya watoto wenye mahitaji maalum, tunajenga shule ya
sekondari ya kidato cha tano na sita, tunajenga Shule ya Sekondari Bulangwa,”
amesema Dkt. Biteko.
Ametaja
miradi mingine ya maendeleo iliyojengwa ni ukumbi mkubwa wa mikutano na kituo
cha afya.
Aidha,
wanatarajia kufikisha umeme katika vitongoji ambavyo havina umeme pamoja na
kukamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa kisasa.
Pamoja na
hayo amewaomba wananchi wa Kata hiyo kumpigia kura diwani nyingi diwani
anayegombea kwa kuwa kwa miaka mitano iliyopita amefanya kazi nzuri.
“ Kama
mbunge ninaridhika mno na kazi inayofanywa na Yusuf kwa sababu anashughulikia
maendeleo ya watu. Nawaomba wana Bulangwa tumpe ushirikiano kwa kumpigia kura
nyingi ili aendelee kutuletea maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea
kusema hakuna maendeleo yanayopatikana bila kupiga kura hivyo amewaomba
wananchi wa Bulangwa 15,504 waliojiandikisha kupiga kura wajitokeze Oktoba 29
na wawachague wagombea wa CCM.
Naye,
Mgombea wa Udiwani Kata ya Katente, Tabu Ngwahani amesema kata hiyo imenufaika na miradi mingi
ya maendeleo kama vile kujenga madarasa katika Shule za Msingi Igulwa, Bomani,
Umoja, Bwenda na Katente.
Amesema kuwa wameendelea kupokea fedha kwa ajili ya
ujenzi wa soko, stendi na uwanja wa mpira.
“
Tunaendelea kuboresha barabara, tulipokea shilingi milioni 300 kwa ajili ya
hospitali. Pia tulipokea shilingi milioni 900 na tumejenga majengo mengine
ikiwemo chumba cha upasuaji,” amesema Nkwandu.
Kwa
upande wake, Mgombea wa Udiwani Kata ya Bulangwa, Yusuf Mohammed Yusuf
amemshukuru Dkt. Biteko kwa kutoa fedha shilingi milioni 350 kwa ajili ya
kujenga Shule ya Kilimahewa.
Amesema
kuwa katika Kata hiyo wanatarajia pia kujenga Shule mpya ya Msingi ya Muungano,
kujenga barabara pamoja na kusogeza umeme katika Vitongoji vya Kilimahewa na
Muungano.




0 Maoni