Tanzania
imetajwa kuwa nchi inayoongoza barani Afrika kwa ongezeko la watalii, kwa
mujibu wa Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN World Tourism
Organization). Taifa hili limepata kutambuliwa kwa kuwa na ongezeko kubwa zaidi
la idadi ya watalii baada ya janga la UVIKO-19, likifikia kiwango cha ukuaji
cha asilimia 48.
Hayo
yameelezwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani, ambayo hufanyika
kila mwaka tarehe 27 Septemba. Kwa mwaka huu, kilele cha maadhimisho hayo
kilifanyika katika Eneo la Hifadhi la Ngorongoro (picnic site).
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, alisema kuwa kiwango
cha ukuaji wa Tanzania kilikuwa kikubwa zaidi kuliko cha Ethiopia (asilimia
40), Morocco (35%), Kenya (11%) na Tunisia (9%).
Aidha,
alieleza kuwa ripoti ya utalii ya mwaka 2025 kutoka UN Tourism imeitaja
Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 20 bora duniani zinazofanya vizuri zaidi katika
sekta ya utalii, kwa wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia 50.
Kati ya
mwaka 2021 hadi 2024, idadi ya watalii wa kimataifa iliongezeka kutoka 922,692
hadi 2,141,895, sawa na ongezeko la asilimia 132.1. Utalii wa ndani pia
uliongezeka kwa kasi kubwa kutoka 788,933 hadi 3,218,352, ongezeko la asilimia
307.9.
Ifikapo
Desemba 2024, jumla ya watalii wa ndani na wa kimataifa ilikuwa 5,360,247,
ongezeko la asilimia 107.2.
Mapato
yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola bilioni 1.3 za Marekani mwaka
2021 hadi dola bilioni 3.9 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 200.
Dkt.
Abbasi alisema mafanikio haya yametokana na jitihada za Serikali katika
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020–2025, ambayo inalenga kufikia
watalii milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 za Marekani ifikapo mwaka ujao.
Kuanzia
Januari hadi Julai 2025, idadi ya watalii iliendelea kuongezeka kwa asilimia
9.2, ikifikia milioni 1.27, ikilinganishwa na milioni 1.16 katika kipindi kama
hicho mwaka 2024.
Aliisifu
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
kwa kuboresha miundombinu, kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano
(TEHAMA), pamoja na kuitangaza Tanzania kupitia filamu kama “The Royal Tour” na
“Amazing Tanzania”, ambazo zimechangia kuiweka nchi katika ramani ya dunia ya
utalii.
Maadhimisho
ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu:
“Utalii na Mabadiliko Endelevu” (Tourism and Sustainable Transformation), ikilenga kuhamasisha ubunifu, taaluma, maendeleo ya biashara na ushirikishwaji wa jamii katika ukuaji wa utalii.





0 Maoni