Tanzania
imeendelea kuibua heshima katika sekta ya ufugaji nyuki baada ya kushiriki
kikamilifu kwenye Kongresi ya 49 ya Kimataifa ya Wafugaji Nyuki (Apimondia)
iliyofunguliwa Septemba 23, 2025 jijini Copenhagen, Denmark, ikihusisha zaidi
ya washiriki 7,000 kutoka nchi 121 duniani.
Ujumbe wa
Tanzania, ulioongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, ulihusisha pia taasisi za utafiti
TaFORI, TAWIRI na TARI pamoja na wadau binafsi akiwemo Grand Apiary, Bee Topia
Tanzania, PMM na Worker Bees Africa. Washiriki hao waliwasilisha tafiti, bidhaa
na mikakati ya kibiashara, hatua iliyoinua hadhi ya taifa katika anga ya
kimataifa.
Sambamba
na kongresi hiyo, maonesho ya kibiashara ya ApiExpo yalifanyika yakihusisha
kampuni 179 kutoka nchi 44, yakionesha vifaa na ubunifu mpya katika sekta ya
nyuki.
Katika
hotuba za ufunguzi, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dk. Qu Dongyu, na Makamu wa Rais wa
Bunge la Ulaya, Martin HojsÃk, walisisitiza umuhimu wa nyuki katika usalama wa
chakula, bioanuwai na maendeleo ya vijijini.
Septemba
24, Balozi wa Afrika Kusini nchini Scandinavia, Mhe. Fikile Sylvia Magubane, alitembelea
banda la Tanzania na kusifu hatua ya nchi hiyo kuuza asali kwenye soko la Umoja
wa Ulaya kwa kuzingatia viwango vya ubora. Hata hivyo, alitaka kufahamu kwa
nini kongresi ijayo ya 2027 haitafanyika tena Arusha.
Akijibu,
Prof. Silayo alieleza kuwa changamoto za ujenzi wa ukumbi mpya wa kimataifa
(MKICC) zilisababisha Apimondia kuhamishia mkutano huo Dubai, Falme za Kiarabu.
Licha ya
mabadiliko hayo, Tanzania imetajwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika
biashara ya asali, huku ikihimizwa kuendeleza ushirikiano wa kikanda ili
kuimarisha nafasi ya bara hili katika soko la dunia.




0 Maoni