Wakala ya
Barabara za Vijijini ma Mijini (TARURA) Mkoa wa Geita inahudumia mtandao wa barabara upatao Km. 7274 na kati ya hizo Km. 564 ya barabara zinazohudumia
maeneo ya madini.
Hayo
yamebainishwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Geita Mhandisi David Msechu wakati
akiongea na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nane ya Madini yanayoendelea
Mkoani hapa.
Amesema
katika mtandao huo asilimia 60 ya barabara zinapitika hivyo maonesho hayo licha ya kutoa elimu kwa
umma,wanashiriki kikamilifu kuhakikisha wanaendeleza ukuaji wa uchumi pamoja na
kuendeleza huduma za jamii kwa kuhudumia barabara zinazoelekea maeneo ya
migodini.
Aidha,
Mhandisi Msechu amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026 wametenga
kiasi cha shilingi milioni 580 kwa ajili ya kukamilisha Km. 210 zikiwemo barabara zinazoelekea migodini.
Kwa
upande mwingine Mhandisi Msechu amesema TARURA Geita wana Maabara ya kisasa
ambayo inapima ubora wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na
miundombinu mingine inayotekelezwa na
Taasisi nyingine zikiwemo TANESCO, Tume ya Umwagiliaji pamoja RUWASA ambayo inatumia maabara hiyo kutekeleza
miradi yao kwa ubora unaohitajika.
Naye,
Mhandisi wa Miradi kutoka TARURA Makao Makuu Faizer Mbange amesema wanatumia
maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya barabara
ikiwemo kutokupitisha wanyama kwenye barabara, kulinda na kutunza barabara,
kuepuka kulima kandokando ya barabara pamoja na kutopitisha mizigo mizito
kwenye barabara.
Amesema
wananchi wengi waliotembelea banda la TARURA baadhi yao walikuwa na changamoto
ya kutoelewa masuala ya fidia hivyo wameweza kutoa elimu hiyo pia.
“TARURA
inatekeleza miradi kwa fedha za ndani pamoja na ile ya fedha za ufadhili hivyo
ipo baadhi ya miradi ambayo ina fidia.”
Ameongeza kusema kwamba TARURA pia imeweza kutoa elimu ya uanzishaji wa vikundi kazi kwa ajili ya matengenezo madogo madogo ya barabara ambapo vikundi hivyo huhusika pia katika ulinzi wa barabara hizo..



0 Maoni