WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iweke utaratibu wa kuziwezesha taasisi
zinazojihusisha na kilimo kwa kuzipatia zana za kisasa za kilimo ili kukuza
sekta hiyo.
Amesema kufanya hivyo
kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija katika shughuli za kilimo
zinazofanywa na taaaisi hizo. “Mitambo hii ya kupandia, kuvunia pamoja na
umwagiliaji ina gharama kubwa sana, lakini Wizara yetu ya Kilimo ikiweka
utaratibu mzuri wa kuziwezesha hata kwa mkopo itazisaidia kuzalisha kwa tija.”
Ametoa agizo leo
(Jumapili, Agosti 03, 2025) wakati akizungumza na wadau wa ushirika na wananchi
waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Kitaifa yaliyofanyika katika
Kijiji cha Ushirika, kwenye viwanja vya maonesho ya NaneNane, Nzughuni, jijini
Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wakulima kwa mwaka 2025.
Amesema taasisi kama
Magereza, JKT ambazo zinafanya shughuli za kilimo zikipatiwa zana hizo kwa
mikopo, zitawawezeshwa kuwa na teknolojia za kisasa jambo ambalo wasingeweza
kulifanya kwa kutumia fedha zao.
Akizungumzia kuhusu
ushirika, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, yaani
misimu ya kilimo ya 2023/2024 na 2024/2025, nchi imeshuhudia mafanikio makubwa
yanayodhihirisha nguvu ya ushirika katika kuleta tija kwenye sekta ya kilimo na
kuinua maisha ya wananchi. Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za
pamoja kati ya Serikali, vyama vya ushirika, na wanachama.
“Katika kipindi hicho,
pembejeo za kilimo zenye thamani ya shilingi trilioni moja zimesambazwa kwa
wakulima kupitia mfumo wa ushirika katika mikoa mbalimbali na pia, tani milioni
3.8 za mazao mbalimbali zenye thamani ya shilingi trilioni 6.2 zimeuzwa kupitia
vyama vya ushirika.
Amesema hiyo ni dalili
kwamba wakulima wameweza kupata masoko ya uhakika na bei nzuri kupitia vyama
vyao na hivyo kuongeza kipato chao na kuimarisha uchumi wa maeneo yao. Ametumia
fursa hiyo kusisitiza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu dhana, historia na
umuhimu wa ushirika katika kuimarisha maisha ya watu kiuchumi na kijamii.
Mapema, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli alisema utendaji wa ushirika nchini uko salama
na umebadilika sana hadi kufikia hatua ya baadhi ya vyama kuweza kununua mazao,
kubangua na kuuza nje ya nchi.
Amesema kutokana na
ufanisi unaoendelea kuonekana kwenye tasnia ya ushirika, Wizara hiyo hivi sasa
inalenga kuongeza thamani na kwamba baada ya miaka mitatu ijayo, inatarajia
kuona baadhi ya SACCOS zinageuka kuwa benki.
Katika hatua nyingine,
Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege amemshukuru Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa kusimamia urejeshaji wa mali za ushirika hali ambayo imechangia
kuimarishwa kwa ushirika nchini.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu
ulikuwa na hamu ya kuona ushirika unafufuka nchini. Timu uliyoiunda ya
kufuatilia mali za ushirika ilifanya kazi nzuri. Sasa hivi baadhi zimeanza
kufanya kazi, kwa mfano kiwanda cha Sola kilichopo Simiyu, viwanda vya KAKU,
Mbogwe na Chato ambavyo tayari vimeanza kuchambua pamba,” alisema.
“Kutokana na kazi hiyo,
na sisi tumejiongeza. Sasa hivi tumeanza kazi ya kutambua mali zote za ushirika
na kuzisajili kwenye mfumo wa kielektroniki ili tujue iko wapi na ni ya nani.
Hadi sasa tumeshasajili mali 4,990 zenye thamani ya shilingi trilioni moja.
Tunataka kabla ya Desemba, 2025 mali zote ziwe zimeshasajiliwa.”
Alisema wameunda Mfumo wa
Usimamizi wa Vyama vya Ushirika Tanzania (MUVU) ambapo hadi sasa, tayari
wameshasajili wanachama milioni nne. “Ulitoa maelekezo tuwe na mfumo ambao kama
tukitaka tuwatambue wanachama wetu iwe rahisi kufanya hivyo; tujue wako wapi,
wanafanya nini na wahitaji pembejeo ya aina gani na ya kiasi gani.”
Kuhusu utekelezaji wa
mfumo wa stakabadhi za ghala, Dkt. Ndiege alisema hadi sasa, vyama vya ushirika
vimeuza mazao yenye thamani ya sh. trilioni nne na idadi ya mazao imeongezeka
na kufikia 14 kutoka matano ya awali. “Mikoa nayo imeongezeka, sasa tunao
Songwe, Shinyanga na Geita ambao wanatumia mfumo huu,” aliongeza.
0 Maoni