Wananchi mbalimbali wameendelea kutembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ili kujionea, kujifunza na kununua bidhaa mbalimbali ambazo zinatokana na mazao ya misitu katika Maonesho ya Nane Nane Jijini Dodoma.
Wananchi wanatembelea
sehemu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na kuona bidhaa hizo ikiwa ni
pamoja na thamani mbalimbali zitokanazo na miti, mianzi na kamba za porini
(hezilani) ambazo zimetumika kutengeneza thamanj hizo.
Wananchi hao wamevutiwa
na ubora na uzuri wa bidhaa hizo ambazo zinatengenezwa hapa nchini kutokana na
mazao mbalimbali yatokanayo na misitu ikiwa ni pamoja na viti, vitanda,
mapambo na thamani nyingi mbalimbali.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wananchi hao wamesema kuwa wamekuwa wakiona thamani kama hizo zikitoka
nje ya nchi na kwasasa zinazalishwa hapa Tanzania kwa ubora wa hali ya juu.
"Kwa sasa
tunajivunia kuwa na bidhaa zetu wenyewe ambazo zinazalishwa hapahapa nchini na
nimeona kwa kweli zina ubora wa hali juu na bei zake ni nafuu sana," amesema
Teddy Masanja.
Mbali na bidhaa na
upatikanaji wa bidhaa hizo, Wataalamu kutoka TFS wanaendelea kutoa elimu ya miche na
upatikanaji wa mbegu bora za miti , fursa ya kujionea shughuli za ufugaji
nyuki, zikiwemo maandalizi ya manzuki, uvunaji na uchakataji wa mazao ya nyuki
na bidhaa zake
Aidha, TFS imewahimiza
wananchi kuendelea kutembelea banda lao katika maonesho ya NaneNane ambayo
yanafanyika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma na katika maeneo mengine nchini
yanapofanyika Kikanda ili kupata elimu zaidi juu ya uhifadhi wa misitu, ufugaji
wa nyuki, pamoja na kupata ofa maalumu za kutembelea vivutio vya utalii wa
ikolojia vinavyosimamiwa na wakala huo.
Maonesho ya Nane Nane
yameanza Agosti 1,2025 na yanatarajiwa kufika kilele chake Agosti 8,2025 yenye
kauli mbiu " Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi 2025".
0 Maoni